Muonekano baada ya kutokea Ajali mbaya ya gari imetokea asubuhi ya saa 3.30, Jumatano March 11,2015 katika kijiji cha Changarawe wilayani Mafinga mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya na kusababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 43 na majeruhi.


Kamanda Mpinga akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa wanahabari (hayupo pichani).

KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini Tanzania , Mohammed Mpinga ametoa tamko kuhusiana na madereva wote waliosababisha ajali kwa uzembe kuwa watafutiwa leseni zao mara moja.

Akizungumza na wanahabari jana April 14,2015 mchana katika Ofisi za Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani jijini Dar es Salaam, Kamanda Mpinga alisema kuwa katika kukabiliana na wimbi la ajali, wamedhamiria kufuta leseni zote za madereva wazembe ili kukomesha ajali zinazoendelea kutokea nchini.

Kamanda Mpinga alisema hivi karibuni kumetokea ajali ambazo miongoni mwa ajali hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva hivyo ni dhahiri kuwa lazima madereva waliohusika kufanya uzembe wafutiwe leseni ili wasiweze kufanya kazi sehemu yoyote ambapo wote wataofutiwa leseni zao, watawaanika katika tovuti mbalimbali ili iwe fundisho kwa wengine.
Baadhi ya wanahabari wakifuatilia mkutano huo.

Alisema kwa upande wa mabasi yanayosafirisha abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine, Kikosi cha Usalama Barabarani kitahakikisha kinazingatia muda uliopangwa wa kufika kituo husika na endapo dereva atakiuka kwa kutozingatia muda atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, Mpinga alitoa rai kwa wananchi wote wanaosafiri katika vyombo vya usafiri kutoa taarifa mara moja pale wanapoona dereva anakwenda mwendo kasi usiozingatia sheria za usalama barabarani.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani wakimsikiliza Kamanda Mpinga (hayupo pichani).


Mwishoni, Kamanda Mpinga alitoa salamu za pole kwa ndugu jamaa na marafiki walioguswa na vifo 103 vilivyotokea kwa kipindi cha Machi mwishoni hadi sasa na kuwataka wafiwa kuwa na moyo wa subira katika kipindi hicho kigumu.

“Watu waliofariki kutokana na ajali hizi toka hiyo tarehe 11 mwezii wa tatu hadi hilo tukio la tarehe 14 takribani mwezi mmoja tu wamefariki watu 103 na kujeruhi watu 38.. katika hao watu 103 wengi ni abiria.. sababu kubwa ya ajali hizi ni makosa ya kibinadamu ambayo kwa kiasi kikubwa ni uzembe wa dereva.“

“Amesema Watu 103 wamepoteza maisha na wengine 138 kujeruhiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Machi 11 hadi Aprili 12 mwaka huu 2015, kutokana na ajali za barabarani.

Kamanda Mpinga alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi sasa, zimetokea ajali nane, vifo 103 na majeruhi 138.

Alisema kwa kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi kumetokea vifo vya watu 866 na majeruhi 2,370 kutokana na ajali hizo.

“Kuanzia Januari zimetokea ajali 823 vifo 273 majeruhi 876, mwezi Februari zimetokea ajali 641, vifo 236 majeruhi 726 na Machi zimetokea ajali 652, vifo 357 na majeruhi 761,” alisema Mpinga.

Alisema baadhi ya matukio makubwa ya ajali hizo ni miongoni mwa ajali mbaya ambazo zilitokea Marchi 11, mwaka huu 2015 katika kijiji cha Changarawe, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa iliyohusisha magari mawili likiwamo basi na lori la mizigo na kuua watu 50 na majeruhi 22.

Alisema Machi 19, mwaka huu 2015 eneo la Mikumi Mbugani mkoani Morogoro, ilitokea ajali iliyohusisha gari aina ya Tata na basi la abiria na kusababisha vifo saba na majeruhi 17.

Aliongeza kuwa Machi 17, mwaka huu 2015 mkoani Morogoro, eneo la Mikumi Mbugani ilitokea ajali kati ya basi na lori aina ya Fuso ambayo ilisababisha vifo vya watu wawili na majeruhi nane.

Alisema Aprili Mosi, mwaka huu 2015 mkoani Morogoro, ilitokea ajali na kusababisha vifo vinne, majeruhi 47 na Aprili 3, mwaka huu mkoani Morogoro Makunganya ilitokea ajali iliyohusisha mashabiki wa Klabu ya soka ya Simba na kusababisha vifo saba na majeruhi 22.

Alisema Aprili 9, mwaka huu 2015 mkoani Tanga katika eneo la Mkata ilitokea ajali iliyosababisha vifo 10 na majeruhi 12.

Aliongeza kuwa Aprili 10, mwaka huu 2015 mkoani Dodoma, ilitokea ajali iliyosababisha vifo vinne na Aprili 12 ilitokea ajali Mkoa wa Morogoro eneo la milima ya Ivori na kusababisha vifo 19 na majeruhi 10.
 
Top