Kiongozi wa wa chama cha
upinzani cha Nigeria jenerali
Muhammadu Buhari ameshinda
kura za urais na kumuondoa rais
aliyeko Goodluck Jonathan
mamlakani kwa ushindi huo wa
kihistoria.
Hii ndiyo mara kwanza katika
historia ya taifa hilo kwa rais wa
nchi hiyo kung'olewa
madarakani na kiongozi wa
upinzani.
Kambi ya Buhari inaongoza kwa
asilimia kubwa dhidi ya kambi
ya mshindani wake Goodluck
Jonathan, na tayari wameanza
kusheherekea ushindi.
Mpaka sasa chama cha APC cha
Muhammadu Buhari kimepata
kura milioni 10.8 katika baadhi
ya majimbo ya kaskazini mwa
Nigeria, hususan katika majimbo
ya Adamawa, Kano na Kaduna,
huku chama cha rais anaye
maliza muda wake Goodluck
Jonathan kikipata kura milioni
11.8 Kusini mwa nchi hiyo
katika majimbo ya Enugu,
Bayelsa na Rivers.
Kwa jumla ya kura
zilizohesabiwa Muhammadu
Buhari anaongoza kwa kura
milioni 15.4 dhidi ya mshindani
wake rais anaye maliza muda
wake Goodluck Jonathan
aliyepata kura 13.3.
Duru kutoka Nigeria zimebaini
kwamba rais anaye maliza muda
wake Goodluck Jonathan
amempongeza kwa simu
Muhammadu Buhari.
Muhammadu Buhari, ni
Muisilamu, mzaliwa wa Jimbo la
Katsina, Kaskazini mwa Nigeria.
Alizaliwa mwaka 1942, Buhari
alikuwa kiongozi wa saba wa
taifa la Nigeria, kati ya mwaka
1983-1985.
Ni jenerali mstaafu aliyepata
mafunzo ya kijeshi nchini
Nigeria, India, Marekani na
Uingereza .
Buhari aliwahi pia kushika
nyadhifa za ugavana, kamishna
wa raslimali ya mafuta,
mwenyekiti wa shirika la umma
la mafuta, na pia mwenyekiti wa
mfuko wa Amana ya Mafuta.
Inasemekana kuwa Buhari ni
mtu kaidi, hakubali kushindwa.
Naye rais anayemaliza muda
wake Goodluck Jonathan, ni
mkristo, anaye toka eneo la
Niger Delta, kusini mwa Nigeria.
Kampeni ya Jenerali Buhari,
ilitilia mkazo mambo kadha,
miongoni mwake utawala bora,
kufufua uchumi, maendeleo ya
miundombinu,umeme na nishati,
kilimo, elimu, afya, ardhi na
usafiri, kuwezeshwa wanawake,
usalama, na ajira. Ingawaje,
uwili wa nafsi yake bado
unazusha masuala , je ni wa
kijeshi au kidemomkrasi?