Basi la NGORIKA lenye namba za usajili T 770 BKW (kulia) likiwa limeharibika vibaya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la RATCO T 274 DCP lililolala na kufunga barabara eneo la Mkata mkoani Tanga jana April 09,2015 na kusababisha vifo vya watu 10 Papo Hapo.
Jinamizi la ajali limeendelea kugharimu maisha ya Watanzania, baada ya jana April 09, 2015 ,Watu 12 kufa katika ajali mbili tofauti zilizohusisha magari manne katika mikoa ya Tanga na Morogoro,Nchini Tanzania.
Ajali hizo zimetokea takribani mwezi mmoja tangu kutokea kwa ajali nyingine ya basi iliyoua abiria 43 mkoani Iringa.
Katika ajali mkoani Tanga iliyoua watu 10 katika eneo la Mkata katika Kijiji cha Mbweni wilayani Handeni Mkoani Tanga, magari matatu yakiwemo gari dogo, mabasi ya NGORIKA na RATCO, yaligongana majira ya saa 5 asubuhi na kusababisha vifo na majeruhi.
Polisi mkoani Tanga kupitia Kaimu Kamanda wake, Juma Ndaki amethibitisha tukio hilo na kusema ajali hiyo iliyotokea katika barabara ya Dar es Salaam kwenda Tanga na Arusha.
Kwa mujibu wa Kamanda Ndaki, gari dogo aina ya Toyota Passo lenye namba za usajili T 628 CXE lililokuwa likiendeshwa na Baba mzazi wa binti mwenye matatizo ya akili aliyekuwa akipelekwa hospitali ya Rutindi, Korogwe, ndilo chanzo cha ajali, kwani dereva wake ailijaribu kulipita lori ili amwahishe binti yake hospitali, ndipo akajikuta anasababisha ajali hiyo.
Anasema wakati gari hilo dogo likijaribu kulipita lori, lilikutana uso kwa uso na basi RATCO lenye namba T 274 DCP na ndipo dereva wa basi hilo akajaribu kulikwepa na kisha kukutana uso kwa uso na basi la NGORIKA lenye namba T 770 BKW na kusababisha ajali iliyoua watu wanane wa basi la NGORIKA akiwemo dereva wake, na wawili, Baba na bintiye waliokuwa kwenye gari dogo.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda Ndaki alisema dereva wa basi la RATCO, lilikuwa likitoka Tanga kwenda Dar es Salaam na basi la Ngorika lilikuwa likitoka Dar es salaam kwenda Arusha, alivunjika mguu na wote kuchomoka na kwamba taratibu za mazishi ya mguu huozinafanywa.
Majeruhi pamoja na wengine waliokuwa na hali mbaya walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Waliokufa kwenye ajali hiyo ni Wanaume watano, Dereva wa gari dogo na Dereva wa basi la NGORIKA pamoja na Wanawake watano .
Kamanda Ndaki alisema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva wa gari dogo ambaye hakuzingatia alama na sheria za barabarani, jambo ambalo limesababisha simanzi na kukatisha maisha ya watu wasio na hatia.
Alisema maiti wa ajali hiyo wamehifadhiwa katika hospitali ya Magunga Korogwe na maiti wote wametambulika majina yao, ingawa hawakutajwa.
HUKO MKOANI MOROGORO.
Watu wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine 48 kujeruhiwa, 12 kati yao wakilazimika kulazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito ya Mikumi, baada ya basi la kampuni ya Happy Nation walilokuwa wakisafiri nalo kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kupinduka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo majira ya mchana jana April 09,2015 na kupoteza uhai wa watu wawili, Mwanamke na Mwanaume ambao hawakuweza kufahamika mara moja.
Alisema chanzo cha ajali ya basi hilo lenye namba za usajili T 618 BDN aina ya Scania ni uzembe wa dereva aliyetaka kulipita gari lililokuwa mbele yake, bila kuchukua tahadhari na alipoona kuna gari jingine linakija kutoka upande wa Iringa aliamua kutanua upande wake zaidi na kujikuta likiacha njia na kupinduka mara tatu.
Hata hivyo, alisema baada ya kutokea kwa ajali dereva wa basi alikimbia eneo hilo na anatafutwa na Polisi. Kwa mujibu wa Kamanda huyo, wengine ambao waliumia kiasi walitibiwa na kuruhusiwa kuendelea na safari zao na kwamba Polisi inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na ajali hiyo.
Machi 12, mwaka huu 2015,mkoani Iringa ,basi la Majinja Express lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam liligongana na lori na kisha likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.
Source:-Habari Leo.