Na Shaaban Ndyamukama.
Mahakama ya ardhi ya Chato Mkoani Geita imetoa kibali kwa kampuni ya TISA ACTION MART kubomoa nyumba ( Pichani ) ilioko katika kiwanja NO. 45 cha Mactilida Kamala (73) kilichopo mjini Ngara Mkoani Kagera baada ya kuuzwa tangu 2013.
Ubomoaji huo umefanyika juzi April 14,2015 mjini Ngara chini ya usimamizi wa jeshi la polisi ambapo mmiliki wa kiwanja hicho Bw Charles Mkombo amesema anahitaji kujenga nyumba katika kiwanja hicho ili kufanya shughuli zake.
Bw Mkombo amesema alinunua kiwanja tangu Desemba mwaka juzi kwa shilingi millioni 14 lakini mmiliki wa nyumba hiyo amekua akikaidi kuondoka ambapo alifungua kesi mahakama ya ardhi iliyoko wilayani chato ili kupata haki yake.
Aidha Bi Mactilida Kamala amekanusha kuhusu uuzaji wa kiwanja hicho na kwamba wana ukoo wenzake wamemzunguka na kukiuza licha ya kusainishwa nyaraka mbalimbali kwa madai atapewa msaada kutokana na kuwa mjane.
Kwa upande wa mtoto wa Mactilida aliyejitambulisha kwa jina la Bashasha Kamala amelaani kitendo cha kubomoa nyumba ya mama yake na kwamba harakati za kuuzwa kwa kiwacha cha mama huyo yeye hakuhusishwa.
Hata hivyo Bw Tuombe Sempiga aliyekuwa na nyaraka za ununuzi wa kiwanja hicho nyingine zikiwa za mahakama ya ardhi ya Chato ambaye ni jirani na kiwanja hicho amesema manunuzi yalifanyika kihalali mbele ya ukoo wa mjane huyo.
Madalali wa kampuni ya TISA ACTION MART iliyo na makao makuu jijini Mwanza wakibomoa nyumba ilioko kiwanja NO. 45 cha Mactilida Kamala (73) kilichopo mjini Ngara mkoani Kagera baada ya kuamuliwa kuvunjwa na Mahakama ya Ardhi wilayani Chato mkoani Geita tangu kiuzwe mwaka 2013.