Watanzania wametakiwa kuacha kuamini kuwa vitendo vya ajali za barabarani zinazoendelea kutokea nchini zinasababishwa na imani za kishirikina na badala yake kila mtu atumie nafasi yake kutokemeza wimbi la ajali hizo.
Mwito huo umetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Transevents Marketing Ltd Peter Nzunda wakati akizungumza na Kijukuu Blog ofisi kwake kuhusu kampeni ya dereva makini inayoratibiwa na kampuni hiyo.

Nzunda amesema kuwa ajali zinazoendelea kutokea nchini kwa sasa hazina uhusiano wowote na mambo ya kishirikana na kwamba ajali nyingi zinasababishwa na uzembe bararani kwa baadhi ya madereva na abiria wachache wanaoshabikia mwendo kasi.
Amesema kuwa kila mtanzania akiwa balozi wa mapambano haya kwa kutoa taarifa sahihi kwa askari wa usalama barabarani juu ya uzembe unaofanywa na baadhi ya madereva na kuacha kushabikia mambo yasiyo ya msingi kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza kama si kumaliza kabisa ajali hizo.

Ameongeza kuwa kampeni nyingi za kupambana na ajali za barabarani hazifikii malengo kutokana na nyingi kufanyika kwa nadharia na si vitendo hali inayopelekea ujumbe kutofika ipasavyo kwa wahusika hususan madereva wanaokuwa barabarani muda mwingi.

Katika kupambana na ajali za barabarani kampuni ya Transevents Marketing Ltd imeandaa tuzo ya dereva bora kupitia kampeni ya Dereva makini yenye kauli mbiu isemeyo Abiria ni haki yako kufika Salama.

 
Top