KWA mara ya kwanza tangu kuwapo jaribio la kumpindua Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kiongozi huyo jana alijitokeza hadharani kuzungumza na waandishi wa habari.
Hata hivyo, licha ya wanahabari wengi kutarajia kuwa atazungumzia jaribio la kumpindua, lakini mazungumzo yake yote hakugusia jambo lolote linalohusu mgogoro wa kisiasa, badala yake alizungumzia tishio la al-Shabaab.

Pamoja na kutozungumzia jaribio hilo pamoja na suala la uchaguzi, hata hivyo mmoja wa wasaidizi wake akijibu swali la waandishi wa habari alisema kuna uwezekano wa uchaguzi wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu, ukasogezwa mbele.

Akiwa mwenye tabasamu na kutulia, Rais Nkurunziza aliwasalimia wanahabari akiwa Ikulu mjini Bujumbura ambako hakuzungumzia kabisa mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Alizungumzia tishio la kundi la kigaidi la Somalia la al-Qaeda lenye uhusiano na wanamgambo wa al-Shabaab waliotoa tahadhari ya kufanya mashambulio nchini Burundi na nchi zingine ambazo zina majeshi yao katika Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Somalia.

“Tumechukua tahadhari dhidi ya al-Shabaab. Tunalichukulia tishio hilo kwa uzito mkubwa sana,” alisema.

Nkurunziza amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa wapinzani wake la kumtaka asigombee kwa muhula wa tatu.


Pamoja na shinikizo hilo wiki iliyopita baadhi ya wanajeshi walijipanga wakati yupo jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano uliokuwa unajadili suala la Burundi.

Alipoulizwa kama uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa, baada ya Rais Nkurunzinza kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari, msemaji wa Rais Willy Nyamitwe, alijibu kuwa kuna uwezekano huo ila Tume ya Uchaguzi ndiyo yenye uamuzi wa kusogeza mbele uchaguzi huo. 

Uchaguzi wa wabunge ulipangwa kufanyika Mei 26, na uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika Juni 26 mwaka huu.

Nyamitwe alisema huenda uchaguzi huo ukasogezwa mbele kwa siku mbili au tatu au wiki. Alisema pia rais ameshutumu shambulizi dhidi ya vituo binafsi vya redio ambavyo vilifungwa wakati wa vurugu za kudhibiti mapinduzi hayo.

“Kuchoma moto vyombo vya habari, kwa rais hili ni jambo ambalo linatakiwa kulaaniwa kwa nguvu zote,” alisisitiza.

Utata wa Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu, umekuwa kiini cha mgogoro wa kisiasa nchini humo, huku wanaharakati na wanasiasa wakipinga hatua hiyo kwa madai kuwa ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani ya mwaka 2006.

Pamoja na kupingwa na waandamanaji kwa takribani wiki mbili, jaribio la mapinduzi na shinikizo la mataifa ya nje, Nkurunziza hana dalili ya kubadilisha mawazo yake ya kugombea katika uchaguzi ujao.

‘Wasaliti’ mahakamani 
Katika hatua nyingine, maafisa 17 wa usalama, wakiwemo majenerali watano wanaotuhumiwa kufanya jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza juzi walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kuyumbisha usalama wa taifa.

Msemaji wa Serikali ya Rais wa Burundi, Gervais Abayeho alisema miongoni mwa watuhumiwa hao ni majenerali watatu wa jeshi na wawili wa polisi, wanne ni maofisa wa vyeo vya chini na nane ni askali.

Kiongozi wa jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa, Meja Jenerali Godefroid Niyombare bado hajakamatwa na bado anatafutwa na maofisa usalama wa nchi hiyo.

Hata hivyo mawakili wa watuhumiwa hao walisema wateja wao wamefanyiwa mateso wakati wakiwa kizuizini.

Wakili mwingine, Cyriaque Nibitegeka, alisema mteja wake, afisa wa jeshi, alilazimishwa kukiri kosa baada ya kuoneshwa mtutu wa bunduki na amegoma kula chakula tangu alipokamatwa.

Hata hivyo, vyombo vya habari vinaeleza kuwa maafisa wa usalama waaminifu kwa Rais Nkurunziza wanaendelea na misako dhidi ya watu wanoshukiwa kuwa `wasaliti’ mjini Bujumbura.

 
Top