Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ 

Kikosi cha Taifa Stars kiliondoka Jumatano kwenda huko kushiriki mashindano hayo yanafanyika katika miji tofauti ambayo kilele chake kitakuwa Mei 30.
Leo, kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinaingia kwenye Uwanja wa Olympia Park, Rustenburg Afrika Kusini kupambana na Swaziland katika mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Cosafa ambayo yalifunguliwa jana.

Kikosi cha Taifa Stars kiliondoka Jumatano kwenda huko kushiriki mashindano hayo yanafanyika katika miji tofauti ambayo kilele chake kitakuwa Mei 30.

Katika mashindano hayo Tanzania imepangwa katika Kundi B na timu za Lesotho, Swaziland na Madagascar, wakati Kundi A lina timu za Namibia, Zimbabwe, Shelisheli na Mauritius.

Tanzania ni mshiriki mwalikwa kama ilivyo kwa Ghana, lakini kutokana ubora wa viwango vya Fifa, Taifa Stars imelazimika kuanzia hatua ya makundi wakati Ghana imepangwa kuanzia moja kwa moja katika robo fainali pamoja na wenyeji Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji, Malawi na Botswana.

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij alisema anataka kutumia mashindano hayo kama sehemu yake ya maandalizi ya michuano ya kusaka kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2017) pamoja na yale ya Chan 2016.

Nooij alisema anajua Swaziland ni timu nzuri na kwamba mara ya mwisho katika mchezo wa kirafiki timu hizo zilitoka sare, hivyo anawaanda vijana wake kupata ushindi katika mchezo huo. Kikosi cha Swaziland kina wachezaji mchanganyiko wakiwamo wanaocheza ligi ya nyumbani na baadhi soka la kulipwa Afrika Kusini.

Tunakubaliana na kauli ya Kocha Nooij kwamba kinachohitajika ni matokeo mazuri kwenye mashindano hayo kwani yatasaidia kuwajenga wachezaji wetu kabla ya kuwakabili Misri, Nigeria na Chad pamoja na Uganda katika kusaka kufuzu kwa fainali za Afrika.

Tunafahamu heshima pekee kwa mchezaji wa timu ya taifa ni kuhakikisha nchi yake inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwa kuhakikisha inafuzu kushiriki mashindano makubwa pamoja na kuchukua ubingwa.

Ushindi unapatikana kutokana na nidhamu na moyo wa kujituma kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja. Hakuna timu inayoweza kufanikiwa kama wachezaji wake watakosa nidhamu ya mchezo na kushindwa kufuata maelekezo ya kocha.

Tunaamini wachezaji wote watakuwa makini kuepuka kupata kadi na kucheza faulo ambazo zitaigharimu timu hiyo katika mashindano hayo muhimu.

Tunawaombea wachezaji wa Taifa Stars wanaoliwakilisha Taifa letu katika mashindano hayo huku tukiamini watatuwakilisha vyema kwa sababu ni mabalozi wazuri.

Tunaamini Stars itashindana kwa nguvu na maarifa ili kuepuka kuwa timu mshiriki tu kwenye mashindano hayo. Pia tunaamini kila mchezaji ambaye atashuka uwanjani au kukaa benchi atakuwa akitambua wajibu wake ipasavyo kwamba ni kusaka ushindi si vinginevyo.

 
Top