Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara Mkoani Kagera Bw Cornel Ngudungi amesema zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura kwenye Daftari la Kudumu wilayani humo limefanikiwa kwa Asilimia 95.4.
Bw Ngudungi amesema zoezi la Uandikishaji wilayani Ngara limemalizika June 20 mwaka huu 2015 na kwamba Watu Laki Moja elfu 24na 82 wenye sifa wameandikishwa.

Amesema awali walitarajia kuandikisha zaidi ya watu Laki Moja na Elfu 30 na kwamba licha ya changamoto mbalimbali zilijitokeza wakati wa zoezi hilo ikiwemo kugoma kufanya kazi kwa Mashine za BVR, Kuishiwa Chaji hasa maeneo ya vijijini pamoja na baadhi ya Raia wa Kigeni kutaka kujiandikisha lakini zoezi hilo limekwenda vizuri

Bw Ngudungi amewahimiza Wakazi wa wilaya ya Ngara kuvitunza Vitambulisho vyao vya Kupigia Kura ili wapate fursa ya kupiga Kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu,2015.

KWA MUJIBU WA OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU imetoa makadirio ya idadi ya watu wanaotarajiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 ambao wanakisiwa kuwa watafikia milioni 24.2nchi nzima.

Taarifa hizo ni makadirio ya idadi ya watu wanaostahili kupiga kura katika majimbo ya uchaguzi Tanzania kwa mwaka 2015. 

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo 2010 walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.

Takwimu hizi zimetolewa katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Jimbo la Uchaguzi na Kata au Shehia kama yalivyokuwa mwaka 2010. Makadirio ya idadi ya wapigakura yametokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Kwa mujibu wa ripoti iliyo kwenye kitabu maalumu cha takwimu za wapiga kura mwaka huu 2015, ambayo nakala yake imepatikana kupitia Ofisi ya Takwimu ya Mkoa wa Arusha, idadi hiyo imepatikana kwa kutumia mbinu za kidemografia zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na uhamiaji katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Majimbo ya Uchaguzi na Kata au Shehia husika.

Inakadiriwa kuwa ifikapo siku ya uchaguzi,2015, Tanzania itakuwa na watu wapatao 48,522,229 ambapo watakaokuwa na umri wa kupiga kura watakuwa ni watu 24,252,927 iwapo wote watafanikiwa kuandikishwa upya.


Mkoa wa Dar es Salaam wenye majimbo nane unatarajiwa kuwa na wapiga kura wengi zaidi watakaofikia milioni 3, ukifuatiwa na Mbeyaitakayokuwa na wapiga kura milioni 1.5, Mwanza milioni 1.4 na Morogoro itakayokuwa na wapigakura milioni 1.3 katika nafasi ya nne.

Mikoa mingine inayotarajiwa kuwa na wapiga kura wengi ni pamoja naKagera itakayokuwa na wapigakura milioni 1.2, Tabora inayokadiriwa kuwa na idadi ya wapiga kura milioni 1.1, Tanga nayo kwa idadi kama hiyo ya milioni 1.1 pamoja na Dodoma itakayokuwa na wastani wa wapigakura milioni moja.

Mkoa wa Kilimanjaro unatarajiwa kuwa na wapiga kura 976,000katika nafasi ya tisa na hatimaye Arusha kufunga kumi- bora ikiwa na matarajio ya wapiga kura wapatao 944,000. 

Idadi ya wapigakura watarajiwa kwa mikoa mingine ni kama ifuatavyo:-

Mara (834,000), 

Geita (808,000), 

Ruvuma (783,000),

Mtwara (773,000), 

Shinyanga (762,000), 

Manyara (741,000), 

Simiyu (714,000), 

Singida, (698,000),

Pwani (644,000), 

Iringa (524,000), 

Rukwa (472,000) 

na Njombe (393,000).

Mkoa mpya wa Katavi, ambao una idadi ya wakazi wapatao 609,000ndio utakuwa na idadi ndogo zaidi ya wapigakura kwa Tanzania bara wakitarajiwa kuwa 271,000.

Huko visiwani mkoa wa Mjini Magharibi unatarajiwa kuwa na wapigakura 347,000, Kaskazini Unguja 104,000, Kaskazini Pemba103,000, Kusini Pemba 95,000 na Kusini Unguja 69,000.

 
Top