Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akisoma hotuba ya kuhimisha mkutano wa 20 wa Bunge mjini Dodoma jana Julai 09,2015. Picha na Emmanuel Herman .
Rais Jakaya Kikwete anamaliza utawala wake kwa kuongeza maeneo mapya ya utawala, baada ya kuridhia kuanzishwa kwa wilaya mpya sitana mkoa mmoja wa Songwe utakaofanya nchi kuwa na mikoa 31.
Akitoa hotuba ya kuahirisha Bunge hadi itakapotangazwa kwenye Tangazo la Serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa Rais Kikwete ameridhia uanzishwaji wa mkoa huo uliomegwa kutoka Mkoa wa Mbeya.
Alisema pia zimeongezwa wilaya mpya sita, zikiwamo Ubungo na Kigamboni za mkoani Dar es Salaam, halmashauri 25 za wilaya, halmashauri 17 za manispaa na miji, tarafa tano na kata 586.
Pinda alisema Serikali imeamua kuanzisha maeneo hayo ya utawala ili kusogeza utawala kwa watu na kuchagiza maendeleo nchini kwa kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Halmashauri za wilaya zilizoanzishwa ni Buchosa, Malinyi, Madaba, Manyoni, Mpimbwe, Nsimbo, Buhigwe, Nyang’wale, Kankonko Uvinza, Mlele, Mbogwe, Buhigwe, Momba, Butiama, Ushetu, Nyasa, Busega, Msalala, Ikungi, Mkalama, Itilima, Ikungi, Bubumburi na Kariua,” alisema Pinda.
Pamoja na halmashauri hizo za wilaya, kiongozi huyo mkuu wa shughuli za Serikali alisema, Serikali imeongeza manispaa na miji mipyaambayo ni Chalinze, Ifakara, Nanyamba, Newala, Kondoa, Mafinga, Mbulu, Bunda, Mbinga, Tunduma, Nzega, Handeni, Kasulu, Geita, Masasi, Manispaa ya Ilemela na Kahama.
“Pia, mheshimiwa rais ameridhia kuanzishwa tarafa tano ikiwemo yaMchemwa iliyopo Newala na tarafa nne za Tandahimba ambazo ni Mchichila, Mihambwe, Mambamba, Namangombya.
“Aidha, tumeanzisha kata mpya 586… mheshimiwa spika inawezekana orodha haijatoa taarifa za kina, lakini tunaweza kuisahihisha tutakapokuwa tunatoa kwenye tangazo rasmi za Serikali siku zijazo,” alisema Pinda.
Katika hotuba hiyo, Pinda alisema kazi ya kuanzisha maeneo mapya hufanywa kila baada ya muda fulani kutokana na mazingira, ongezeko la watu pamoja na vigezo mbalimbali na anaamini litazidi kuimarisha utendaji na shughuli za maendeleo nchini.
Pinda pia alitumia hotuba hiyo kueleza mafanikio mbalimbali ya Serikali ya awamu ya nne katika sekta zote huku akisisitiza kuwa wataongeza jitihada za kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuongeza mapato nchini.
Kuhusu uandikishaji wapiga kura, Pinda alisema hadi sasa kazi hiyo imekamilika katika halmashauri za mikoa 13 ya Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Dodoma, Katavi, Rukwa, Singida, Tabora, Kagera, na Kigoma.
Alisema Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) imevuka lengo kwa kuandikisha watu 11,248,194 wenye sifa za kupiga kura na malengo ya Tume ni kuandikisha kati ya watu milioni 21 hadi 23.
Source:-Gazeti la Mwananchi Julai 10,2015.