Wanafunzi wapatao 21 wanaosoma Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Kata ya Kala mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, wamefukuzwa shule kwa muda usiojulikana kwa kuvaa viatu maarufu yeboyebo.
Imeelezwa kwamba yeboyebo hizo zilikusanywa na kuchomwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kunatokana na waraka uliotolewa na Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Msingi) ukipiga marufuku wanafunzi kuvaa aina hiyo ya viatu shuleni.
Hata hivyo,jana Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi (Msingi), Misana Kwangula, alikanusha kutoa waraka huo kwa shule hiyo.
“Sina taarifa rasmi ila jana jioni (Jumatatu) alinipigia simu mkazi mmoja akinitaarifu kwamba kuna mwalimu wa shule ya msingi Kilambo cha Mkolechi amechoma moto viatu vya wanafunzi kwa madai kuwa ofisa elimu (msingi) ametoa waraka kwamba wanafunzi hawatakiwi kuvaa yeboyebo shuleni…
“Hakuna waraka wala marufuku yoyote iliyotolewa, isitoshe sio sahihi hata kidogo wala sio kitu kizuri kuchoma vifaa walivyonavyo wanafunzi…. Sasa kama amewachomea wanafunzi hao viatu hivyo vya yeboyebo basi awanunulie viatu vya ngozi,” alisema Kwangula.
Mkasa huo wa wanafunzi hao kufukuzwa shule na kuchomewa yeboyebo walizovaa ulitokea juzi wakati wanafunzi hao walipofika shuleni wakiwa wamevaa viatu hivyo.
Inaelezwa kwamba mwalimu wa zamu, Baraka Mwakasege aliwazuia kuingia darasani, badala yake akawaamuru wavue viatu vyao.
Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, baada ya hatua hiyo, mwalimu huyo wa zamu alizikusanya yeboyebo na kuzitia kiberiti kisha akawafukuza wanafunzi hao kwa muda usiojulikana hadi wazazi na walezi watakapowanunulia viatu vya ngozi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Posian Ally alikanusha kumtuma mwalimu wa zamu kuwafukuza wanafunzi hao shule kwa muda usiojulikana wala kuteketeza kwa moto yeboyebo zao.
Alisema ataitisha kikao ili kujadili suala hilo na kwamba mwalimu huyo akibainika kutenda kosa hilo ataamriwa kuwanunulia watoto hao viatu vingine.