Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza kwenye mkutano wa kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Dk Magufuli tangu aanze kazi amekuwa akipambana na ufisadi katika sekta za umma, jambo ambalo limesababisha viongozi na maofisa kujikuta wakisimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema anayoyafanya Rais John Magufuli kupambana na ufisadi walimuandalia utaratibu wa kikatiba, lakini Bunge Maalumu la Katiba (BMK) likauondoa.
Dk Magufuli tangu aanze kazi amekuwa akipambana na ufisadi katika sekta za umma, jambo ambalo limesababisha viongozi na maofisa kujikuta wakisimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu.
Jaji Warioba alisema hayo jana kwenye mkutano wa kitaifa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015, ulioandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao ni waangalizi wa ndani wa uchaguzi.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini ambaye alikuwa msemaji mkuu kwenye mkutano huo, alisema: “Kama kuna kitu kinaumiza roho ni kuondolewa kwa miiko ya uongozi kwenye Katiba Inayopendekezwa. Anachokifanya Rais Magufuli ndicho walichokipendekeza wananchi ili kupambana na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi.”
Mapema kabisa, wakati akianza kuzungumza, waziri mkuu huyo wa zamani alitahadharisha kuwa katika tathmini yake hatozungumzia uchaguzi wa Zanzibar, kwa sababu unahitaji muda na mjadala wa peke yake. Hivyo akajikita katika uchaguzi wa Bara tu na kueleza mengi aliyoyashuhudia ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na wadau wote wanaoshiriki.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi ambao kwa pamoja walijadiliana juu ya mfumo wa kisheria na kitaasisi uliowezesha uchaguzi wa mwaka 2015, ushiriki wa vyama vya siasa, vyombo vya habari na makundi maalumu, asasi za kiraia na athari zitokanazo na uchguzi huo.
Akijikita kwenye mada hizo, Jaji Warioba alifafanua masuala muhimu ambayo alipendekeza yafanyiwe kazi ili kuongeza wigo wa demokrasia nchini. Akikumbuka hamasa iliyokuwapo alisema ‘haijapata kutokea,’ akitumia kauli ya rafiki yake wa kitambo, marehemu Moses Nnauye.
“Kulikuwa na mwitikio mkubwa sana ambao ulichagizwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Watu wengi walijitokeza katika hatua zote, kama walivyofanya kwenye kutoa maoni ya Katiba ndivyo walivyoshiriki harakati za uchaguzi,” alisema.
Vyama vya siasa
Alikumbushia ripoti ya Umoja wa Ulaya (EU) ambayo ilieleza kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa uhuru, haki na usawa kwamba hakumaanisha kuwa hapakuwa na kasoro kwenye mchakato mzima.
Alisema mchakato wa kuwapata wagombea ndani ya vyama ulikuwa na malalamiko mengi ambayo yanapaswa kushughulikiwa na viongozi wakuu wa vyama husika.
Alitoa mfano kwa chama tawala: “Wakati wa kutafuta wadhamini mikoani ilikuwa ni kama wagombea hao wapo kwenye kampeni za uchaguzi. Walikuwa na misafara mirefu kiasi cha kuwaaminisha wananchi kuwa wangepitishwa. Hii ilisababisha baadhi kuchepuka na kuongeza hamasa baada ya kujiunga na upinzani.”
Mlezi wa vyama hivyo ambaye pia ni msajili, Jaji Francis Mutungi aliwaasa wadau hao kwa kueleza kuwa baadhi ya vyama havikuwa na ilani ingawa viliruhusiwa kushiriki, hivyo kuvitaka kukuza demokrasia na uwazi ili kuongeza mshikamano baina ya wanachama na viongozi wao.
“Tujenge tabia ya kukubali matokeo ya uchaguzi na kuepuka kuhamasisha wanachama kushiriki masuala yanayovunja sheria. Ni wakati sasa, vyama vya siasa viache kuandaa vikundi vya ulinzi na jukumu hilo liachwe kwa vyombo husika kwani linaleta sintofahamu kwa wananchi kwa kudhani kuwa kutakuwa na machafuko,” alisema Jaji Mutungi.
Gharama za uchaguzi
Jaji Warioba alionya juu ya matumizi makubwa ya fedha kuendesha mchakato wa uchaguzi, kwamba huko mbele unaweza ukaleta makundi ya wanaostahili na wasiofaa kuchaguliwa endapo hatua stahiki hazitochukuliwa kuyadhibiti.
“Katika kuimarisha demokrasia, ndani ya vyama ndiko kuna matatizo mengi ingawa hatutaki kuyasema. Gharama za uchaguzi zinavipendelea vyama vikubwa pekee, vidogo vinaumia na bado viongozi wa vyama hawatendi haki kwa wote. Ni rahisi kwao kuilalamikia tume ya uchaguzi, lakini ukiangalia wanachokifanya ni tofauti na madai yao,” alisema.
Aliyekuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki na Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alisema viongozi wana kazi kubwa ya kuimarisha demokrasia ndani ya vyama vyao ili kujenga imani kati yao na wanachama.
Wakati Jaji Warioba akisema kuwa uchaguzi umekuwa bidhaa adimu kutokana na gharama zake, Cheyo alieleza: “Vyama vingi havina msingi wa fedha na uwezekano uliopo ni kuwa mwenye hela ndiye mwenye nafasi kubwa ya kupitishwa. Rushwa haikudhibitiwa mwaka jana, wapo baadhi ya wagombea waliwapa watu ‘pesa ya chai’ majukwaani.”
CREDIT: MWANANCHI