Zaidi ya magari 1,500 jana, yalikwama katika eneo la Chalinze Nyama wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa zaidi ya saa 10, baada ya mafuriko kuziba barabara kuu itokayo Dodoma kwenda Morogoro. 
Mafuriko hayo yalitokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku mbili mfululizo. 

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitakuwa katika eneo hilo ili kutoa ushauri kwa watumiaji wa barabara na kuwataka wananchi kufuata ushauri wa vyombo hivyo. 

“Wakazi wanaoishi mabondeni wahame ili kuepusha athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha,”alisema. 

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema zaidi ya kaya 100 zimekosa mahali pa kuishi baada ya maji kujaa ndani ya nyumba zao. 

“Kaya mbili zilichelewa kutoka kwenye nyumba wanazoishi ikabidi tutafute Kikosi cha Zimamoto ambacho kilifika na kuwaokoa,”alisema. 

Mgomi alisema mafuriko katika sehemu hiyo yanatokana na daraja dogo lililopo ambalo linashindwa kuhimili wingi wa maji. 

Kufuatia tukio hilo, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, viongozi wa halmashauri, tarafa na kata walitarajiwa kukutana jioni kwa ajili ya kuangalia jinsi ya kuwasaidia waliokumbwa na maafa. 

“Tuone wadau wanatusaidiaje, tunapataje chakula lakini watu wa Msalaba Mwekundu wamefika na mablanketi na baadhi ya vifaa,” alisema.
 
Top