Kwa ufupi
Shitindi alisema hayo kwa waandishi wa habari baada ya mkutano wake na kamati ya kudumu ya kutatua kero na changamoto za sekta ya usafirishaji kwa njia ya barabara, iliyoundwa baada ya kutokea mgomo wa madereva Februari mwaka jana.
Dar es Salaam. Serikali imeanza kuyaondoa matuta yaliyowekwa kwenye barabara kuu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano waliyowekeana na madereva wa malori.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ajira, Erick Shitindi kwamba sehemu zilizokuwa na matuta badala yake zitawekwa alama za vivuko kwa watembea kwa miguu.
Shitindi alisema hayo kwa waandishi wa habari baada ya mkutano wake na kamati ya kudumu ya kutatua kero na changamoto za sekta ya usafirishaji kwa njia ya barabara, iliyoundwa baada ya kutokea mgomo wa madereva Februari mwaka jana.
“Wakati wa mgomo moja ya kero za madereva walizoziwasilisha kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda ni uwepo wa matuta katika njia kuu, hivyo basi tayari Serikali imeanza kuondoa matuta hayo na inataraji kuyamaliza kabisa mara baada ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017,” alisema Shitindi.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Fortunatus Musilimu alisema matuta hayo yaliwekwa kwa shinikizo la wananchi, hasa pale inapotokea ajali lakini kanuni za barabara kuu haitakiwi kuwa na matuta.
“Tutaendelea kuweka mabango makubwa ya maelekezo na alama za barabarani, kila mahali na njia ya kuepuka ajali za barabarani, siyo uwepo wa matuta bali kila mmoja kufuata kwa usahihi kanuni za usalama barabarani,” alisema Musilimu.
Alisema lengo la matuta hayo ilikuwa kupunguza ajali na kunusuru uhai wa wananchi, lakini imekuwa kinyume kwani baadhi yamegeuka kuwa chanzo cha ajali kutokana na namna yalivyowekwa.
Mwenyekiti wa chama cha madereva, Shaabani Mdemu alisema pamoja na hatua hizo, bado kuna changamoto ya mikataba ya madereva itakayoweka wazi mishahara na posho zao.