Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro leo,April 18,2016.
Katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais alimnukuu Baba wa Taifa, Mwl Julius Nyerere akisema kuwa nia ya Mwenge wa Uhuru tangu mwanzo ni kumulika mipaka ya nchi yetu dhidi ya maadui, kuleta matumaini pale ambapo hakuna matumaini, kuondoa chuki pale ambapo kuna chuki na kuleta heshima pale ambapo kuna dharau.

Alisema nia hiyo ya kuwepo kwa Mwenge wa Uhuru kama alivyomnukuu Baba wa Taifa, inaendana na dhana ya kutumbua majipu katika Serikali ya awamu ya tano. 

Alisema utumbuaji majipu unalenga kuleta matumaini kwa wananchi ambao wamekata tamaa na kuleta heshima kwa wananchi waliodharauliwa.

“Kaulimbiu ya mbio ya za mwenge mwaka huu ni hii: Vijana ni nguvu kazi ya taifa, washirikishwe na wawezeshwe,”alisema Makamu wa Rais na kuongeza kuwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa hawajatumika ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali.

Alizitaja baadhi ya sababu au changamoto zinazowakabili vijana nchini kuwa ni ukosefu wa ajira, uwezo mdogo wa kuajiri kwenye soko la ajira, ukosefu wa mitaji rafiki kwa vijana, maeneo ya kufanyia kazi pamoja na mitazamo hasi kwa baadhi ya vijana kwa kuchagua kazi.

Makamu wa Rais pia amewataadharisha vijana kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ukimwi na matumizi ya madawa ya kulevya.

Amesema vijana wenye umri kati ya miaka 16 -24 ndiyo wanaongoza kwa kuathiriwa na maambukizi ya ukimwi.

Amesema athari za ukimwi na madawa ya kulevya kwa vijana ni kubwa lakini pia zinaongeza mzigo kwa jamii na serikali katika kuwatibu, kuwahudumia na kuongezeka kwa vifo.

Kwa upande wake, Waziri Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, amemtambulisha George Jackson Kijimba kuwa ndiye kiongozi wa mbio za mwenge mwaka huu akisaidiana na wakimbiza mwenge wengine watano.

Alisema sherehe za kuhitimisha mbio hizo za mwenge wa uhuru zitafanyika mkoani Simiyu tarehe 14 Oktoba mwaka huu,2016.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa mbio za Mwenge kwa mwaka 2016 George Jackson Mbijima kutoka mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kukimbiza mwenge huo katika Mikoa na wilaya zote za Tanzania.Picha na OMR.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Taifa kwenye Sherehe za uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa zilizofanyika leo april 18, 2016 katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.

Mwenge wa Uhuru umezinduliwa rasmi mbio zake ili kukimbizwa katika halmashauri za wilaya na Manispaa zipatazo 179 za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani.

Baada ya kuwashwa leo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kuhitimishwa wilayani Gairo ambako Aprili 25, mwaka huu,2016 utakabidhiwa mpakani mwa wilaya hiyo na Kilindi ya Mkoa wa Tanga ili kuendelea na mbio zake.

Mwenge wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza Desemba 9, 1961 kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro, kutimiza ahadi ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai Uhuru wa Tanganyika.

 
Top