Aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Kuyani Mkunjera (36), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, kwa kupokea mshahara wa jeshi hilo huku akiwa ameacha kazi kwa kipindi cha miezi saba.
Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Antony Ngowi alisema mshtakiwa alijinufaisha pasipo kufanyia kazi kitu anachonufaika nacho na alipokea fedha kiasi kinachozidi Sh4.6 milioni ambayo ni kinyume cha kifungu cha 23 (1) (a) cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sheria namba 11 ya mwaka 2007.
Ngowi alisema mshtakiwa kuanzia Oktoba 12, 2015 hadi Aprili 28, mwaka huu alijipatia kiasi hicho cha fedha kwa kujinufaisha pasipo kukifanyia kazi kitu anachonufaika nacho, huku akiwa siyo mfanyakazi wa jeshi hilo na akiwa ameajiriwa na taasisi nyingine.
Mshtakiwa alikana shitaka hilo na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyomtaka awe na kiasi cha Sh3 milioni za ahadi na wadhamini wawili wenye barua za kuwatambulisha, vitambulisho na picha za paspoti.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 23, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.