Polisi mkoani Mwanza imebaini mtandao unaohusika na ujambazi wa kuvamia, kupora, kujeruhi na kuua wafanyabiashara wa maduka ya fedha. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tayari wamewatia mbaroni watu watatu wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo wakiwa na bunduki aina ya SMG ikiwa na magazine nne na risasi 144. 

Pia, watuhumiwa hao walikutwa na kofia moja ya kuficha uso, hijabu mbili, jaketi moja pamoja na mabegi mawili wanayotunzia silaha zilizokuwa zimefichwa kwenye nyumba wanayoishi. 

“Polisi bado inaendelea kumsaka kinara wa mtandao huu (jina linahifadhiwa), ambaye alifanikiwa kukwepa mtego wa polisi, tunawaomba raia wema kutoa taarifa zitakazofanikisha kumtia mbaroni,” alisema SACP Msangi. 

Alisema bunduki iliyokamatwa inaaminika kutumika katika matukio zaidi ya sita ya uporaji katika maduka ya fedha. 

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema vyombo vya dola tayari vimebaini mitandao saba ya uhalifu mkoani Mwanza. 

Kitwanga ambaye pia ni mbunge wa Misungwi aliwaeleza wapigakura wake kuwa tayari mitandao miwili kati ya hiyo saba ilikuwa imeangamizwa, huku jitihada za kuangamiza iliyosalia zikiendelea.
 
Top