Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.
Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.
Msengi alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.
Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema;“Tumechoshwa na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.
Hata hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.
Alilaani kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.
Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.