Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amesema atamsindikiza kiongozi wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo katika makao makuu ya uhamiaji Tanzania.
“Nitampeleka Abdul Nondo Uhamiaji tarehe 20/4/2018 kwa mamlaka yangu kama Mbunge wa Kigoma Mjini. Wananchi wa Kigoma Mjini waliopo Dar watakaotaka kunisindikiza Mbunge wao kumpeleka Abdul huko sitawazuia. Anyways, Mwami lazima asindikizwe,” alisema zito katika ukurasa wake wa Twitter.
“Siku hiyo Uhamiaji watatuambia kama Kigoma sio Tanzania ili tuwaombe wasio wa Kigoma warudi Tanzania maana haiwezekani waliowengi pasiwe kwao na wachache ndio iwe kwao,” aliongeza Zitto.
Hii ni baada ya taarifa iliotoka kutoka mtandao huo ambao ulieleza kuwa Bw Nondo alipata barua ya kuitwa na uhamiaji ili 'akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake.'
Taarifa hizo zilisema 'afisa uhamiaji mkoa alitamka kuwa sheria inawaruhusu kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka uraia wake. Na kuwa wanamashaka na uraia wa Abdul Nondo,hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania.'