ASILI YA NGARA

Wilaya ya Ngara ni wilaya inayopatikana Mkoa wa Kagera kasikazini magharibi mwa Tanzania, wilaya hiyo inakaliwa na wahangaza na washubi ambapo wilaya hiyo inapakana na nchi za Rwanda na Burundi na lugha ya watu hao ni kihangaza na kishubi ambapo lugha hizo zinaingiliana na lugha za nchi hizo mbili na kuwafanya wenyeji kuelewana kilugha na wakazi wa mataifa hayo jirani.

 Mti aina ya Umunyinya uliopandwa Halmashauri ya wilaya ya Ngara
Jina la asili la wilaya ya Ngara kabla ya kuitwa Ngara iliitwa Kibimba (yaani pori). Chanzo cha jinna hilo la Ngara lilitokana na sehemu iliyokuwa maalumu kwa mikutanao ambayo ilifanyika chini ya miti mikubwa inayoitwa iminyinya yingara( ilikuwa miti mikubwa yenye matawi yaliyosambaa) ambapo kwa sasa eneo hilo ndipo ilipo halmashauri ya wilaya ya Ngara na mti wa kumbukumbu upo mpaka sasa.

Mti wa Umunyinya uliopandwa halmashauri ya wilaya ya Ngara ambao asili yake imebeba jina la Ngara.
Wilaya ya Ngara ilikuwa na watawala wa kichifu ambapo kulikuwa na machifu wa pande mbili yaani chifu wa Bugufi na Chifu wa Bushubi. Machifu waliotawala Bugufi walikuwa Balamba wa kwanza, Rusengo, Ruvubi, Mpanda, Kanyamazinge na Balamba motto waKayamazinge. Machifu hao wa Bugufi walikuwa wakikutana eneo la Nyamilama ili kupeana maadili na mbinu za kiutawala mfano lilivyo bunge la Dodoma kwa sasa. Na Bushubi alikuwepo chifu Nsoro.

Baadhi ya asili ya majina ya maeneo mbalimbali ya wilaya ya Ngara

Murgwanza awali iliitwa Mugwanza ikiwa na maana eneo lisilokuwa na kitu hivyo hali yake ilikuwa na upepo uliowavutia wamisionari kujenga eneo hilo kanisa, hospitali na makazi yao na kushindwa kutamka jina hilo la asili ndipo wakawa wanatamka Murgwanza na mpaka sasa panaitwa hivyo.

Nyamiaga ilitokana na upepo mkali ambapo wakazi wa eneo hilo walipanda miti na migomba kupunguza upepo huo.

Kabanga ilitokana na sehemu iliyotumika kutengeneza zana za vita kama upinde na mshale sababu eneo hilo lilikuwa na miti ya kutengeneza zana hizo iliyojulikana kama imibanga. Hayo ni baadhi ya maaeneo tu ya wilaya ya Ngara na ni ngumu kuchambua maeneo yote.

UTAMADUNI

Mila na desturi ya wahangaza na washubi, mtoto alikuwa haruhusiwa kukaria kiti cha baba yake wala kula sahani moja na wazazi wake hivyo walitengwa pembeni na kula peke yao.


Wahangaza walikuwa hawaruhusiwi kula kondoo na mbuzi bali kondoo na mbuzi waliliwa na kabila duni lijulikanalo kama watwa ( mbuzi aliitwa impene kwa kilugha kwa sababu waliichukulia kama ipo uchi na ndio sababu ya kutoliwa na kabila hilo enzi hizo.

picha ya mbuzi aliyekuwa haramu kuliwa enzi hizo lakini kwa sasa ni nyama safi

Imani ya wahangaza na washubi (dini) ilikuwa ni kuabudu chini ya miti ya Milumba (ikivumu) waliabudu mungu aliyeitwa kilanga kilumwelu (mungu wa amani) na pia kutambikia kwenye vijumba vidogo vilivyoitwa Indalo. Aidha wakazi hao waliamini kinga za asili za chale na hirizi.

Picha ya mti wa mulumba (ikivumu)

Msichana akibeba mimba nje ya ndoa adhabu yake ilikuwa ni kufungwa jiwe la kusagia ana kutupwa mto Ruvubu eneo lililojulikana kama Mmasangano (Nyaburumbi). Na adhabu nyingine ilikuwa ni kumfungia sagio (jiwe la kusaga) na kuwekwa njiapanda (amayilabili) ili aliwe na wanyama mpaka kufa.

Picha ya jiwe la kusagia
Wahangaza walitumia tiba ya asili yaani miti shamba kwa magonjwa. Pia kuondoa mizimu iliyokuwa inawasumbua watu alikuwa anatafutwa mbuzi au kuku mweupe wa kafara na mgonjwa kuruka kafara hiyo kasha kutupwa porini kwenye miti iitwayo imilinzi.
wazee wa asili na waliochangia kuandaa historia hii
Utamaduni wa kuoana ilikuwa ni kwamba kijana hakuruhusiwa kutafuta mchumba bali wazazi wake walimchagulia mchumba kwa kuangalia historia ya ukoo au familia anakotoka mchumba husika. Wazazi wa pande zote mbili walikubaliana kwa kupeana mahari (posa) ya jembe la mkia (jembe la asili) au nguo zilizotengenezwa kutokana na magome ya miti (ikibugu). Binti alipelekwa usiku kuolewa.

Mahusiano ya watu yalidumishwa kwa kutembeleana baada ya kuandaa pombe ya asili yaani impeke na gwagwa. Kulikuwa na aina mbili ya unywaji wa pombe hii, aina ya kwanza watu walialikwa na kujumuika sehemu moja walipoitwa na familia iliyoandaa pombe hiyo hasa hasa msimu wa mavuno (kiangazi) kwa kilugha illiitwa gutumila na pia njia nyingine ilikuwa ya kwenda na mitungi ya pombe kutembelea familia Fulani( kwa kilugha kugemula). Wanawake na watoto walizuiliwa kunywa aina za pombe isipokuwa walikunywa pombe ya ndimasi au iliyochakachuliwa (umushalulo).
 mitungi ya pombe
Burudani ya kabila hizo ni miaeleko yaani ngoma ya asili ya wilaya ya Ngara.
Ngoma ya mieleko kama burudani asilia  ya Ngara

Shughuli kuu ya kabila hili ilikuwa kilimo, ufugaji kwa kiasi na uwindaji wa wanyama.

Watoto walirithishwa mila na wazazi wao kwa kupewa elimu ya vitendo na hasa kugawa kazi kwa kuzingatia mgawanyiko wa kazi kijinsia.

MAJINA YA ASILI YA KIHANGAZA

Majina yalitokana na matukio mbalimbali yaliyozikumba familia husika mfano Nduhiye, Luchamumikani, Semagogwa na Nyantuntu. Hayo majina na mengineyo yalitokana na wanafamilia kukubwa na balaa Fulani kwa kipindi kirefu mfano kuzaa watoto na kufariki bila kukua.

Majina ya mungu (kilanga)
Gwankuba
Mhindakazi
Mlengela
Kashana
Mahobeka
Ruboha
Ndundagi
Na mengineyo

Majina ya kihangaza (majina ya asili)

Kwa mtoto wa kwanza hadi wa tano hawakupewa majina hayo ya kimila. ( hii inaonesha wazee wetu walitambua uzazi wa mpango tangu mwanzo maana walitakiwa kuzaa watoto wasiozidi watano.) kuanzia mtoto wa sita na kuendelea walipewa majina yafuatayo:-
Wa sita aliitwa Miburo
Wa saba aliitwa Gwasa
Wa nane aliitwa Minani
Wa tisa aliitwa Nyabenda
Wa kumi aliitwa Machumi
Wa kumi na moja aliitwa Misago
Wa kumi na mbili aliitwa Kalenzo
Wa kumi na tatu aliitwa Kasongero
Wa kumi na nne aliitwa Ndululutse
Wa kumi na tano aliitwa Myandagalo
Wa kumi na sita aliitwa Misezero
Wa kumi na saba aliitwa Nkunkumuye
Wa kumi na nane aliitwa Ntiboye
Wa kumi na tisa aliitwa Choniki
Wa ishirini aliitwa Bujana
Wa ishirini na moja aliitwa Sebilele
Wa ishirini na mbili aliitwa Bisakumbwa
Wa ishirini na tatu aliitwa Bifutso
Wa ishirini na nne aliitwa Semyavu
Wa ishirini na tano aliitwa Ntamazina

Hapo mzazi alikuwa anafunga kizazi hivyo akiendelea kuzaa alikuwa anaanza upya kwa jina la Butanguye kwa mtoto wa kike na Ndatagunye kwa mtoto wa kiume.

Mzee Essau Hosea (kulia) akiwa na Jeremia Nduhiye Bunamiye (yupo hai mpaka sasa) (wazee waliochangia kuelezea historia hii ya Ngara)

HISTORIA YA JINA LA HANGAZA
Kabila la hangaza au wahangaza ni kabila lililopo wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera nchini Tanzania, ni kabila la watu wapole, wastaarabu na wakarimu kwa wageni. Ila si vema leo tukajua asili ya neno au jina hangaza lilitokana na nini au wapi lilitokea.

Mzee Essau Hosea (kulia) akiwa na Mzee Singirankabo Sugwigano( alifariki 2012 akiwa na miaka 120) (wazee waliochangia kuelezea historia hii ya Ngara)

Kwa historia ya mababu zetu ni kwamba hapo zamani kulikuwa na watemi wawili wa nchi mbili tofauti yaani Burundi na Rwandakwa sasa , watemi hao walikuwa mtemi Mwambutsa wa Burundi na mtemi Kigeri wa Rwanda. Watemi hao wawili walikuja kupigana na mtemi Kinyamazinge wa Ngara. Watu wa Ngara walibuni vita ya kupigania mpakani(boarder defensive) ambapo mababu zeetu walishinda mchana kutwa wakikata miti na usiku ambao ndo ulikuwa muda wa vita walikoka moto mkubwa, sasa wale warundi na wanyarwanda walipokuja kupigana vita vya ana kwa ana( full force attack) walishangaa kuona Moto wakati muda huo wapiganaji wa ngara yaani mababu zetu wakiwa tazama vizuri na kuwapiga mishale kwa urahisi sababu ya mwanga wa moto ndipo neno hangaaza likiwa na maana ya tazama kwa umakini kwa lugha ya Kiswahili lilianzia pale maana warundi na wanyarwanda hawakuweza kuwaona vizuri wapiganaji wetu maana walikuwa kando kidogo na moto huo hivyo wakawa wanaambiza hangaaza neza ulibe yo bali yaani angalia kwa makini uone walipo kwa kiswahili . Na pia kipindi hicho lilitumika zaidi kumaanisha mwanga wa vita kuanzia hapo wenzetu wa Burundi na Rwanda baada ya kushindwa vita hiyo ndipo walipoanza kutuita wahangaza. Na ndipo msemo wa kilugha unasema utazi umhangaza amuhanga amaso ulipoanzia.

Mzee Essau Hosea (kulia) akiwa na Mzee Benjamini Sigaye(wazee waliochangia kuelezea historia hii ya Ngara)

Wazee wengine wa Mubinyange waliochangia kuelezea historia hii baadhi yao walishaaga dunia

Imechapishwa na Ezra Essau kwa usaidizi wa historia kutoka kwa Essau Hosea Chiza.

Kwa ushauri na maoni au kuongezea kilichosahaulikatutumie kwa email yetu: ezraessau@gmail.com

BONYEZA HAPA LIKE UKURASA WETU UWE UNAPATA HABARI MOJA KWA MOJA
 
Top