Padri akiuombea mwili wa marehemu Prisca Paul Rugeiyamu kanisani.
STORI: WAANDISHI WETU/Uwazi
MFANYABIASHARA mwanamama aliyetambulika kwa jina la Prisca Paul Rugeiyamu au Mama Koku (34) ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi nje ya geti la nyumba yake huku mwanaye Careen (12) akishuhudia. 
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Januari 12, mwaka huu saa mbili usiku maeneo ya Tabata Segerea jijini Dar ambapo kwa mujibu wa chanzo, Prisca alikuwa akirejea nyumbani kwake ndani ya gari aina ya Vitz baada ya kukusanya mapato yake ya siku kutoka kwenye biashara zake.
Mwili wa marehemu ukishushwa kaburini.
Akiwa nje ya geti la nyumba yake akisubiri kufunguliwa, ndipo majambazi walitokea ghafla wakiwa kwenye pikipiki na kulizunguka gari hilo na kutoa bastola wakitaka wapatiwe fedha na laini za mitandao ya simu alizokuwa akizitumia katika biashara yake ya huduma za kifedha kwa njia ya simu katika moja ya maduka yake.
Waombolezaji wakiwa ni wenye huzuni kaburini.

Chanzo hicho kilisema kuwa, Prisca alibishana na majambazi hao kwa muda ambapo walimpiga risasi ya mguuni na kumuongeza nyingine baada ya kuendelea kugoma kutoa fedha.
“ Walimpiga risasi nyingine sehemu za tumbo na kuchukua fedha zinazodaiwa kufikia shilingi milioni arobaini na tano huku mwanaye Careen akishuhudia tukio hilo baada ya kufungua geti hilo kwa ajili ya kumpokea mama yake,” kilisema chanzo.

Waombolezaji wakiweka taji la maua kwenye kaburi la marehemu.
Inaelezwa kuwa Careen baada ya kuona hayo alikimbilia kwa bibi yake ambaye ni mama mzazi wa Prisca anayeishi jirani na nyumba yao aliyefika eneo la tukio ambapo majambazi hao waliokuwa wakijiandaa kutoweka walimpiga risasi ya mguu mama huyo na kuondoka kwa kasi.
Hata hivyo, baada ya majirani kufika eneo hilo walimchukua Prisca na kumkimbiza Hospitali ya Amana lakini alifariki akiwa njiani na maiti yake ikahifadhiwa hospitalini hapo.
 
Mtoto wa marehemu akishika picha ya mama yake.

Akizungumza na waandishi wetu, ndugu wa familia hiyo anayejulikana kwa jina la Geofrey Frank alisema kuwa baada ya kifo chake walishangaa kuona wafanyabiashara wa madini wakija katika msiba na kudai kuwa Prisca alikuwa mfanyabiashara mwenzao, na kuongeza kuwa marehemu hakuweka wazi kazi yake hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo marehemu alikuwa mfanyabiashara wa madini, mmiliki wa duka la vocha za jumla, duka la vifaa vya ujenzi na mmiliki wa duka la vinywaji maeneo ya Segerea.

 
Marehemu Prisca Paul Rugeiyamu enzi za uhau wake.
 
Amewaacha yatima watoto watatu, mkubwa ana miaka 12 huku wengine ni mapacha wana miaka saba. Mwili wa marehemu ulizikwa Januari 15, mwaka huu katika Makaburi ya Segerea jijini Dar.
Imeandaliwa na Shani Ramadhani, Deogratius Mongela na Chande Abdallah.
 
Chanzo: Globalpublisher
 
 
Top