Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Tony Laiser, katika kambi ya Nyarugusu
KAMBI ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma imepokea waomba hifadhi 4,146 kutoka Burundi wanaoikimbia nchi yao kufuatia vurugu za kisiasa kufuatia hatua ya Rais Piere Nkurunzinza, kuteuliwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwania muhula mwingine wa urais.

Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Tony Laiser, amesema mpaka kufikia Mei 6 mwaka huu kambi ya Nyarugusu imepokea na kuwaandikisha waomba hifadhi 4,146 tangu walipoanza kuingia nchini kupitia eneo la Kagunga mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Alisema kuwa jana tarehe 5 walipokea waomba hifadhi 635 na leo asubuhi wamepokea wengine 614, walioletwa na Meli ya MV Liemba kutoka eneo la Kagunga, Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

“Kagunga idadi bado inaendelea kuongezeka na tunaendelea kulifanyia kazi namna gani ya kuweza kuwaokoa wale waomba hifadhi na kuwapeleka mahali panapohusika kwa maana ya kambi ya Nyarugusu,”alisema Laiser.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya waliokimbia nchini mwao ni wanawake na watoto, lakini kwa siku tatu zilizopita wameanza kupokea idadi kubwa ya vijana wengi wao wakiwa wanafunzi.

Akizungumzia suala la raia hao kutoka Burundi kupewa hadhi ya ukimbizi, Laiser, alisema kuwa hilo litategemea na hali ya kiusalama pamoja na kusubiri maelekezo ya viongozi kutoka mamlaka za juu.

Kuhusu uwezo wa kambi ya Nyarugusu kuhifadhi wakimbizi, mratibu huyo wa wakimbizi alisema kuwa uwezo wake ni kuhifadhi watu elfu 50, lakini mpaka sasa hivi idadi hiyo imezidi na kwamba serikali itaangalia ni wapi watawahifadhi.

“Suala hili linaangaliwa, kwa sababu ni suala la kisera. 

Linaangaliwa kwamba idadi itakapokuwa imezidi basi kuangalia uwezekano wa utaratibu mwingine ni wapi watu hawa watahifadhiwa.”

Credit: Kigoma 24hours blog

 
Top