AMA kweli ukishangaa ya Babu wa Loliondo, utayaona ya Mtagata. Katika Mkoa wa Kagera, katika Msitu wa Mtagata, ulioko wilayani Kyerwa, kunapatikana maji yanayoelezwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwamba ni maji ya ajabu. 
Simulizi za baadhi ya wananchi hao, zinaeleza kwamba maji hayo yamekuwa yakitumiwa na jamii ya wakazi wa eneo hilo la Mtagata na maeneo mengine ya jirani, kwa malengo na madhumuni kadhaa, ikiwemo tiba ya magonjwa mbalimbali. 

Kwa mujibu wa simulizi hizo, chanzo hicho cha maji kimegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ya chanzo hicho cha maji yanapatikana maji ya moto muda wote, wakati sehemu ya pili yanapatikana maji baridi muda wote pia. 

Maji hayo yamegawanywa na wakazi hao katika sehemu kuu tatu katika mtumizi ambapo ipo sehemu ya watoto, sehemu ya wanawake na sehemu ya tatu ambayo inatumiwa na wanaume. Watu wenye matatizo mbalimbali ikiwemo magonjwa wanaamini kuwa wakilala kwenye maji hayo kwa dakika kadhaa wanapona maradhi yanayowasumbua. 

Inaelezwa kwamba kinachovutia zaidi katika chanzo hicho cha maji, ni kuyaona maji yakiwa yanachemka na kutoa mvuke kana kwamba huko chini yatokako kuna moto unaochochewa ili kuyachemsha maji hayo. 

Hali hiyo ya maji hayo kuwa ya moto muda wote, inaelezwa kuwavutia zaidi watoto wanapendelea kuyachezea na kuoga maji hayo, kiasi cha kuvuta umati mkubwa wa watu, hasa siku za Jumamosi na Jumapili. 

Mmoja wa watoto anayependa kuoga maji hayo ya moto, ameiambia FikraPevukuwa wengi wao wanapendelea kuoga maji hayo kwa kuwa kuwepo kwake, kunawafanya wasilazimike kuchemsha maji ya kuoga katika kipindi cha majira ya baridi. 

Baadhi ya wenyeji wa eneo hilo, akiwemo aliyejitambulisha kwa jina la Jorida Origines, anasema kuna wakati maji hayo yanakuwa ya moto sana kiasi cha kuweza kuunguza ngozi ya binadamu. 
Katika mahojiano yaliyofanywa na FikraPevu na baadhi ya wakazi wa eneo, imethibitika kuwa baadhi yao hutumia maji hayo kujisafisha na nuksi ili kuepuka kukumbwa na mabalaa mbalimbali katika maeneo yao ya majumbani na makazini kwao. 

Kwa mfano, mkazi mmoja wa kijiji cha Katera, Daniel Moses (43), anasema yeye aliwahi kusubuliwa na matatizo ya maumivu ya mara kwa mara ya mgongo, lakini baada ya kulala usiku kucha katika maji hayo, matatizo yake hayo yalitoweka. 

Kutokana na kivutio hicho cha aina yake kinachotokana na maajabu ya chanzo hicho cha maji, baadhi ya wananchi hao wameishauri Serikali kulifanya eneo hilo kuwa la kitalii ili liweze kuwa na manufaa ya kiuchumi kwao na taifa pia. 

Ofisa wa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Thomasi Mahenge, anakiri kuwepo mambo mengi ya ajabu katika eneo hilo la Msitu wa Mtagata. Anasema tayari ofisi yake imechukua hatua ya kuandika andiko kwa ajili ya kuliwasilisha wizarani ili eneo hilo liweze kutambuliwa katika maeneo ya hifadhi za Taifa. 

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba vivutio vingi vya utalii vinavyotambuliwa katika Taifa hivi, vingi vinapatikana kaskazini mwaTanzania. Vivutio hivyo ni pamoja na Ngorongoro, Serengeti na Mlima Kilimanjaro, vinavyopokea asilimia 90 ya watalii wotekutoka nje. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amekaririwa akisema kuwa baadhi ya maeneo ya kitalii nchini, hasa ya Kitulo, Ruaha, Selous na Katavi hayajatangazwa kiasi cha kutosha kama yanavyotangazwa maeneo hayo ya kaskazini. 

Ripoti ya sita ya hali ya uchumi iliyotolewa hivi karibuni na Benki ya Dunia, imeelezea changamoto kadhaa ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ili sekta ya utalii iwanufaishe Watanzania walio wengi, ambapo moja ya changamoto hiyo ni kupanua vivutio vya utalii na kuvitangaza. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inazo maliasili nyingi ambazo zinaweza kuendeleza sekta hiyo ya utalii kwa kuwa tayari zinafahamika vyema kimataifa, na kwamba karibu kila mwaka, maliasili hizo huchapishwa na kutangazwa katika gazeti la New York Times la nchini Marekani. 

Taarifa ya ripoti hiyo, imebainisha kwamba takriban wageni milioni moja kwa mwaka 2013 waliingia nchini na kuliingizia Taifa dola za Marekani bilioni 1.5, kiasi ambacho ni kikubwa kwa hali yoyote ile ikilinganishwa na Pato Ghafi la Taifa (GDP). 

Wananchi mbalimbali waliobahatika kuchangia ripoti hiyo ya Benki ya Dunia katika mtandao maarufu wa kijamii wa JamiiForums na ukurasa wake waFacebook, wamesema fedha nyingi katika sekta hiyo zinaishia kwenye mikono ya viongozi wasio waaminifu hali inayopelekea Watanzania washindwe kunufaika kupitia sekta hiyo.


Source:-Fikra Pevu.
 
Top