Wagombea wa CCM na Chadema wanaendelea kuchuana vikali kwenye mbio za urais baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza matokeo ya majimbo 113. 
Hadi jana jioni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na NEC, mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alikuwa anaongoza kwenye majimbo mengi akifuatiwa na Edward Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chadema, akiungwa mkono na vyama vingine vitatu vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi. 

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya NEC, Dk Magufuli alikuwa amekusanya zaidi ya kura 2.4 milioni sawa na asilimia 57 katika majimbo hayo, wakati Lowassa, aliyehamia Chadema mwezi Julai, amepata kura zaidi ya 1.7 milionisawa na asilimia 41. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, ni NEC pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo ya urais. 

Mgombea pekee mwanamke kwenye uchaguzi huo kati ya makada nane kutoka vyama tofauti, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, anafuatia nyuma ya wagombea hao wawili, akiwa amepata zaidi ya kura 27,000 ambazo ni sawa na asilimia 0.64. 

Mgombea urais wa ADC, Chifu Lutasola Yemba anamfuatia kwa kuwa na asilimia 0.52 ya kura zote, chini yake akiwapo Hashim Rungwe wa Chaumma ambaye amekusanya asilimia 0.38 ya kura zote. 

Janken Kasambala, anayegombea urais kwa tiketi ya NRA, amekusanya asilimia 0.09 ya kura zote, Macmillan Lyimbo, aliyesimamishwa na TLP (asilimia 0.07) na Fahmy Dovutwa wa UPDP (asilimia 0.07). 

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, ambaye awali aliwahi kusema watatangaza mshindi ndani ya saa 72 baada ya kumalizika upigaji kura, jana aliwaomba wasimamizi wa uchaguzi kuongeza kasi ya kuwatumia matokeo ili wayatangaze. 

Hata hivyo, vyama vinavyounda Ukawa jana vilitoa tamko la pamoja vikidai kuwa uchelewashwaji wa matokeo unatokana na uchakachuaji unaofanywa na kikundi cha chama tawala. 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kura zote zinazokusanywa kutoka majimboni, hupitia hoteli moja Dar es Salaam ambako kuna kikundi hicho na vijana ambao wanachakachua matokeo kabla ya kuyatuma NEC. 

Lakini Jaji Lubuva amekuwa akijitetea kuwa NEC inatangaza matokeo kadri inavyoyapokea na hawana njama zozote dhidi ya chama chochote cha siasa. 

Kwa upande wa matokeo ya ubunge, CCM ilikuwa imeshinda katika majimbo 135, Chadema majimbo 34, CUF majimbo 22, NCCR-Mageuzi jimbo moja na ACT- Wazalendo jimbo moja kati ya 264.
Chanzo-Mpekuzi blog
 
Top