Watu wanne wa familia moja wamefariki dunia kwa kukatwa katwa kwa mapanga huku mtu mmoja akijeruhiwa vibaya mwilini mwake na watu wasiojulikana kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Tukio hilo ambalo limeacha simanzi na huzuni kwa wananchi wa kitongoji cha Iteja kata ya Bugalama wilaya na Mkoa wa Geita, limetokea juzi saa nne usiku.Waliouawa ni watu wa familia moja ya marehemu Samwel Masebu ambao ni Sophia Sylivester (40) Mkulima mkazi wa kitongoji cha Nyabalasana, Mariam Lusafisha (48) mkulima mkazi wa kitongoji cha Iteja(mke wa marehemu), Shinje Honela msukuma mkazi wa kijiji cha Kijiji cha Kishinde na Masanyiwa Malongo ambaye ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.
Watu hao wanadaiwa kuuawa kwa mapanga kwa kile kilichoelezwa kuwa ni imani potofu za kishirikina.
Malunde1 blog ilifika katika kitongoji hicho na kukuta umati wa watu ukiwa umekusanyika katika familia ya Samwel Masebu (marehemu), aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Bugalama lakini alifariki dunia Novemba 12 mwaka huu ambapo kifo chake ndicho kinachohusishwa na masuala ya kishirikina na kusababisha mauaji hayo ya watu wanne wa familia yake.
Inaelezwa kuwa kifo cha Samwel Masebu aliyefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu hivi karibuni alikuwa amerogwa na familia yake(mke wake Mariam Lusafisha) akishirikiana na watu wengine wakiwemo waliouawa.
Diwani wa kata hiyo Luponya Masalu pamoja na viti maalumu Veronica Gelegele wamelaani kitendo hicho na kuliomba jeshi la polisi kuchunguza tukio hilo la kinyama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Lotson Mponjoli amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi hilo la polisi linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kuhusika kwa tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Wananchi wameliomba jeshi la polisi Mkoa wa Geita kuhakikisha wanaokomesha mauaji haya ambayo yalikuwa yamekwisha kwa kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya vinavyohusika.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita