Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilayani ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele, amepiga marufu matumizi ya daraja linalounganisha kijiji cha Bugarama kilichoko katika tarafa ya Rulenge, na kijiji cha Muruyungu kilichoko nchini Burundi, mpaka makubaliano rasmi yatakapofikiwa.
Mwenyekiti huyo Lt. Col. Mntenjele amefikia uamuzi huo hivi Karibuni baada ya wakandarasi wa Burundi kujenga daraja hilo bila ridhaa ya ujenzi wa daraja hilo kati ya Tanzania na Burundi.

“Matumizi ya daraja hili ni marufuku kwa pande zote mbili; hakikisheni halitumiki, tukikuta linatumika pande zote mbili mtawajibika.” Alisema Lt. Col. Mntenjele.

Amesema kujenga daraja hilo bila ridhaa ya pande mbili ni kinyume cha taratibu za ujirani mwema, kwani mipaka rasmi inajulikana, ambayo ameitaja kuwa ni Rusumo, Kabanga na Murusagamba.

Amesema daraja hilo si tatizo tu kwa kuvusha magendo na kuingiza wahamiaji haramu tu, bali pia linaikosesha serikali mapato kwa kupitisha vitu kinyemela.

Aidha, amesistiza kwamba kilichopigwa marufuku ni matumizi ya daraja na siyo ujirani mwema, hivyo, shuguli nyingine zote ziendelee kama kawaida. 

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama Lt. Col. Mntenjele ameabatana na wajumbe wote wa kamati hiyo kukagua daraja hilo lililojengwa na Burundi bila ya ridhaa ya upande wa Tanzania.


CREDIT: MWANAWAMAKONDA BLOG




 
Top