BODI YA MIKOPO YAFUNGUA MILANGO KWA WANAFUNZI WANAOTARAJIA KUJIUNGA NA VYUO VIKUU...

Bodi  ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imefungua maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Taasisi za Elimu ya Juu zinazotambulika kwa masomo ya shahada mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2014/2015. 
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema maombi ya mikopo ambayo yanafanyika kwa njia ya mtandao (Olas) yamefunguliwa kuanzia Aprili 23 na yatafungwa rasmi Juni 30, mwaka huu.
 
Mwaisobwa alisema kuwa Bodi inatarajia kupokea maombi ya mikopo kutoka kwa waombaji wenye sifa zilizoainishwa kwenye mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 ambao ulitolewa na Bodi na kutangazwa kupitia magazeti na tovuti yake mwanzoni mwa Aprili, 2014.
 
Mwongozo huo unataja sifa za msingi za waombaji mikopo kuwa wawe ni wahitimu wa kidato cha sita, Stashahda na cheti cha elimu ya ufundi ((Tvet) hatua ya sita, waliohitimu masomo yao kati ya mwaka 2012 na mwaka 2014 wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu na wanaotarajia kuomba mikopo toka Bodi ya Mikopo wanafahamishwa kuwa wanapaswa kutuma maombi yao ndani ya kipindi kilichotajwa hapo juu. 
Bodi inatarajia kutoa mikopo kwa wanafunzi takriban 35,000 wa mwaka wa kwanza watakaodahiliwa kujiunga na masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.
 
“Pamoja na kupewa fursa ya kuomba mikopo, waombaji wa mikopo wanapaswa kuzingatia masuala ya msingi yanayoambatana na mchakato mzima ikiwa ni pamoja na kusoma kwa umakini mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 kabla ya kulipa ada ya maombi na kujaza fomu, kusoma kwa umakini na kujaza vipengele vyote vya fomu kulingana na maelekezo ili kuiwezesha Bodi kupata taarifa sahihi za mwombaji,” alifafanua Mwaisobwa.
 
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa mwombaji mkopo kuambatanisha nyaraka zinazohitajika kama vile cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini na uthibitisho wa nyaraka kutoka kwa mamlaka husika na mwisho kutuma fomu kamili na viambatanisho kwenye Bodi ya Mikopo ili ziweze kupitia kwenye mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo kwa wakati. 
Aidha, Mwaisobwa alieleza kuwa kuna mabadiliko machache yamefanyika ambapo wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo hawatakiwi kujaza tena fomu kuthibitisha uhitaji wao wa mikopo kwa mwaka unaofuatia.
 
 

CHANZO: NIPASHE
 
Top