Mahakama nchini Sudan imemhukumu kifo mwanamke mmoja anayedaiwa kubadili dini yake na kuolewa na mwanamume mkristo.
Daktari
Mariam Yahya Ibrahim Ishag, ambaye babake ni muisilamu alishitakiwa kwa kosa la
kuasi dini pamoja na kufanya zinaa kwa kuolewa na mwanamume mkristo , kitu
ambacho dini ya kiisilamu imeharamisha kwa wanawake.
Mariam mwenye umri wa miaka 28
pia ni mjamzito na ataadhabiwa kwa kuchapwa mijeledi miamoja kwa kosa la zinaa.
Maafisa
wakuu wanasema kuwa licha ya Mariam kulelewa kwa njia ya kikristo yeye bado ni
muisilamu kwa sababu hiyo ndiyo dini ya babake.
Alipewa
siku tatu baada ya kuhukumiwa aweze kurejea katika dini ya kiisilamu lakini
akakataa na ndio maana adhabu ikasalia.
Kwa
kawaida wanawake waisilamu hawaruhusiwi kuolewa na wanaume wakristo ingawa
wanaume waisilamu wanaruhusiwa kuwaoa wanawake wakristo.
Shirika
la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International linasema kuwa Bi
Ishag alilelewa kama Mkristo muorthodoxi kwa sababu babake hakuwepo naye
maishani mwake.
'Kesi
ya kwanza'
Kesi ya Ibrahim ni ya kwanza ya
aina yake kusikika nchini Sudan , kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Wanaharakati
wa kutetea haki za binadamu, wamelaani uamuzi huo wa mahakama na kuitaka
serikali ya Sudan kuheshimu haki na uhuru wa watu kuabudu.
Maafisa
wa balozi za mataifa ya magharibi pia wamekemea vikali kesi hiyo na kuelezea
asiwasi wao kuihusu.
Maafisa
hao wamewataka maafisa wa sheria nchini humo kuangalia kesi hiyo upya na
kuhakikisha kuwa Mariam anatendewa haki.
Waziri
wa mawasiliano amesema kuwa sio Sudan peke yake ambako sheria za kiisilamu
zinafuatwa na ambako sio sawa kwa mtu kubadili dini yake, hali hiyo pia ipo
nchini Saudi Arabia na katika nchi zingine zinazofuata sheria za kiisilamu.
Serikali
ya Rais Omar al-Bashir inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa
hasa baada ya kujitenga na Sudan Kusini ambako mafuta yake yalikuwa yanatoka
mwaka 2011.