ALICHOKISEMA JK KUHUSU MWANAE KUKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA NCHINI CHINA
RAIS Jakaya Kikwete amesema ni mkusanyiko wa upuuzi kudai kuwa alishiriki kumwokoa mtoto wake, Ridhiwani, aliyedaiwa kukamatwa na dawa za kulevya nje ya nchi.
Alisema urais ni taasisi kubwa nchini na hivyo hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo baadhi yao wanamsukuma ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
“This is nonsense (huu ni ujinga), na ni mkusanyiko wa upuuzi, sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” alisema Kikwete wakati alipokuwa akizungumza na Watanzania waishio Marekani alipokutana nao Agosti 2, mwaka huu mjini Washington D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa nchini Marekani, alisema hayo wakati akijibu maswali kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi mwaka juzi, na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
“Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania,” aliongeza.
Pia alipoulizwa kuhusu kutiliana saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China, ikiwa kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete alikanusha vikali kwa kusema hawezi kufikia suala kama hili kwani kufanya hivyo ni kuiweka nchi rehani.
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria kuiweka rehani, haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri, hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania,” alisisitiza.
Mwaka jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Sikonge mkoani Tabora, alisema kuwa alipata taarifa ya uhakika kutoka China kuwa vijana wenye asili ya Afrika walikamatwa katika uwanja wa ndege wa Hong Kong, wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni 4.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema mkuu wa kitengo cha dawa za kulevya katika uwanja huo alitaja majina ya vijana hao, likiwemo jina la kijana anayedaiwa kuwa wa kigogo katika Serikali ya Rais Kikwete.
Alisema anamtaka Rais Kikwete akanushe uvumi huo kwa kuwa habari zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaihusisha serikali yake.