BODABODA ZAIDI YA 100 WAVAMIA KITUO CHA POLISI USIKU NA KUJERUHI ASKARI..!!
Bodaboda 100 wavamia kituo cha Polisi na kuwajeruhi Askari
Kundi la waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 100 , wamevamia kituo cha Polisi cha kata ya Kiroka wilaya ya Morogoro mkoani Morogoro na kuzusha vurugu.
Hatua hiyo inadaiwa imetokana na kuchoshwa na vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa na askari wa kituo hicho vya kuwakamata na kuwageuza kitega uchumi wanapokuwa hawana makosa.
Mmoja wa wakazi wa kata hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kundi hilo la bodaboda hao lilivamia kituo hicho juzi saa 2 usiku kwa nia ya kutaka kumtoa mwenzao, Ally Musa (19).
Alidai Musa alikamatwa na mmoja wa askari wa kituo hicho mchana kwa tuhuma za kubeba zaidi ya abiria mmoja maarufu kama mishakaki.
Alidai askari huyo alimuomba Musa ampe kitu kidogo, lakini alikataa ndipo akachukua pikipiki yake na kuipeleka kituoni hapo bila ya dereva huyo.
Alidai ilipofika saa 1 usiku dereva huyo alikwenda kituoni hapo kuulizia sababu ya kukamatwa kwa pikipiki yake na kuwekwa rumande .
Alidai baada ya waendesha bodaboda wenzake kupata taarifa, walikusanya wakiwa na silaha mbalimbali, yakiwamo matofari ,mapanga na malungu na kuvamia kituo hicho wakishinikiza atolewe.
Alidai askari hao walionekana kuzidiwa nguvu na kuamua kufyatua risasi za moto hewani na moja kumjeruhi mwenzao, Hamad Kinole, mkazi wa kijiji cha Mkuyuni.
Aliendelea kudai kuwa mwenzao huyo, alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu huku askari huyo akikimbia kusikojulikana .
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema kuwa lilitokea juzi Alasiri katika kijiji cha Mkuyuni baada waendesha bodaboda hao zaidi ya 30 wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki kuvamia kituo hicho kwa nia ya kumtoa mwenzao huyo.
Paul alisema mwenzao huyo ambaye alikuwa akiendesha pikipiki aina Farcon, aliitelekeza baada ya kukamatwa na polisi kwa kubeba abiria watatu.
Alisema askari aliipeleka kituoni pikipiki hiyo na kwamba ilipofika majira ya saa 1 usiku Mussa alifika akitaka apewe na kukamatwa na askari kisha kuswekwa rumande.
Alisema baada ya saa moja kupita lilitokea kundi la waendesha bodaboda wakiwa na malungu, mapanga na matofari wakishinikiza mwenzao huyo aachiwe na kuzusha vurugu na kumjeruhi mguuni PC Edson.
Alisema baada ya kupata taarifa alituma Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kwenda kudhibiti vurugu hizo katika kituo hicho.
Alisema baada ya kudhibiti vurugu hizo, askari hao walibaini mwendesha bodaboda, Kinole (26) amejeruhiwa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kisha kukimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro.
Alisema wanawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kuvamia kituo hicho na kufanya vurufu.
Paul aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Varentino John (18), Jafari Hussein (20), Kulwa Kessy (32) Rashid Idd (22), wakazi wa Kinole.
Wengine ni Mashaka Deresa (20), Juma Ally (30), Hamis Juma(28) wa Kahindu, Shamuna Maneno (19) na Bilal Tamimu (19) wa Kinole.
Alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.
CHANZO: NIPASHE