Jopo la madaktari katika hospitali ya rufaa ya mkoani Manyara kwa kushirikiana na polisi wamefanikiwa kumnasa mkazi wa jijini Dar-es-salaam Bw Godlove Sozigwa akituhumiwa kuomba kufanya mazoezi ya kutibu kwa muda kama daktari wa magonjwa ya moyo na figo kwa kutumia vyeti bandia wakati akitambua kuwa yeye si mtaalam wa tiba.
Bw Godlove Sozigwa kabla ya kukamatwa kwake asubuhi kufuatia jopo hilo la madaktari kubaini kuwa vyeti alivyoviwasilisha katika hospitali hivyo julai 31 ni bandia na hata hivyo alipoitwa na kufanyiwa mahojiano amedai huku akionyesha ukomavu wa kujieleza taaluma hiyo aliipatia katika chuo cha sayansi, tiba na utafiti cha Muhimbili na kufuzu hata hivyo alibahatika serikali kumpeleka nchini India kwa mafunzo zaidi kusomea dawa zaidi.
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoani Manyara Dr Peter Mshali akizungumza na ITV baada ya kukabidhiwa kwa polisi ili kufanyiwa upelelezi amesema katika mahojiano na jopo la madaktari walibaini vyeti hivyo ni bandia aidha pia mtuhumiwa Dr huyo Godlove Sozigwa si mtaalam kulingana na maelezo yake bali ni tapeli na hatari endapo angebahatika kupata nafasi hiyo.
Nae kamanda wa polisi mkoani hapa afande Deusdedit Nsimeki amekiri na katika mahojiano amesema polisi imebaini baada ya kumfanyia mahojiano na upekuzi kumkuta na kompyute mpakato(laptop) muhuri wa kuchonga wa hospitali ya rufaa ya Muhimbili, koti na vyeti mbalimbali,lakini wanafanya upelelezi zaidi kabla ya kumfikisha mahakamani.
Tangu awali ITV iliyoshughudia mtego huo mapema asubuhi na baada ya mtuhumiwa Godlove Sozigwa kufikishwa polisi amekiri kuwa yeye si daktari aliyesoma chuo hicho cha Muhimbili bali anafanya hivyo kutokana na mazingira magumu, hasa kwa kuipenda taaluma ya udaktari baada ya kujifunza katika kituo cha tiba cha Neptune cha matabibu ya kichina kilichopo Ubungo Plaza jijini Dar-es-salaam na kupata uzoefu.
chanzo: itv