Jinamizi la kupingana na kazi iliyofanywa na tume ya marekebisho ya katiba imeendelea kuchukua nafasi nyingine katika Bunge Maalum la katiba kufuatia baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kutumia muda wao kumshambulia aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Mh Jaji Joseph Warioba wakimtaka sasa apumzike kazi yake imeisha.
Wakichangia katika marekebisho ya rasimu ya katiba ambayo imekwisha tolewa na bunge hilo, Mh John Komba ametumia muda wake mwingi wakati akichangia kumshambulia Mh Warioba kuwa analiingia bunge hilo.
Kama vile haitoshi Mh John Cheyo naye alisima na kumtaka Mh Warioba aachane na harakati anazotaka kuzianzisha na badala yake atuliye bunge hilo limaliziye kazi yake.
Kwa upande wake Mh Makame Mbarawa na ambaye ni waziri wa mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia amependekeza suala la mawasiliano liwe ni lamuungano ili kuepusha misuguano ambayo inaweza kutokea.
Akifanya majumuisho ya michango hiyo mwenyekiti wa kamati ya uandishi, Mh Andrew Chenge amesema wamepokea mapendekezo yote jambo kubwa ni wananchi wajaribu kusoma rasimu zote mbili.
Katika hatua nyingine katibu wa Chadema mkoa wa Mara Bw Chacha Heche amejikuta yupo mikononi mwa Polisi alipojaribu kupita karibu na jengo la bunge akitokea Dar es salaam kuelekea mkoani Mara huku akipeperusha bendera ya chama hicho.