Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.
Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano.
“Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.
“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,”alisema.
Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato ukaanza upya.”
Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.
Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa kuwa si mambo ya muungano.
Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.
Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba alisema,“Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata mimi nimeanza kukata tamaa.”
Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya Katiba wanayoitaka.
Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba pia alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi anapumua Katiba’. Dk Mvungi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake.
Maadili ya Viongozi wa umma
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema, “Wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi. Kutokana na maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.”
Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa ambayo ni; utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa (Kiswahili ).
“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa aenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.
Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na maadili ya taifa, kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi wanavyoenzi misingi mikuu na tunu.
Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka miiko ya uongozi kwenye Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.
“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi. Sijui kwa nini Bunge la Katiba wameondoa hili,” alisema.
Madaraka ya Wananchi
Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba kuondoa kipengele cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhishwi na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri ili aweze kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .
“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao wanataka watumie madaraka yao,” alisema.
Mgawanyo wa madaraka
Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya Bunge, Serikali na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais na mawaziri kutoka kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.
“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia, New Zealand,” alisema.
Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini baadaye Rais alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge likalazimika kubadili uamuzi.
“Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa sehemu ya bunge ni kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema.
Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili kutenganisha madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya wamefanya hivyo. Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.”
Muungano
Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar na 10 za Tanzania Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha madaraka ya rais kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni magumu kubadilika kwa upande wa Zanzibar.”
Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au zaidi ya Wawakilishi.