Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema anapokea meseji za simu zaidi ya 50 kwa siku za kumtukana na kusisitiza ataendelea kupambana kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana.
Sitta alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana wakati akielezea kutoridhishwa kwake na kile alichodai ni namna hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Saed Kubenea inavyopotoshwa na wanaomchukia.
“Kuna baadhi ya vyombo vya habari wananichukia mimi binafsi. Wasichanganye chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalumu,”alisema Sitta na kuongeza;
“Mimi napokea matusi kila siku. Meseji zisizopungua 50 viongozi wa Chadema wameweka namba zangu katika tovuti nitukanwe kila siku hilo mimi niko tayari na mnaniona niko safi tu wala sihangaiki nalo.”
“Lakini sasa Bunge Maalumu ni chombo cha kikatiba, kiko tofauti na mwenyekiti wake. Huwezi kuliadhibu Bunge Maalumu kwa sababu hupendi sura ya mwenyekiti wake,” alisema.
Sitta alienda mbali zaidi na kusema, “Kwa hiyo wale wanaoendeleza hayo mapambano tuendelee na tutaendelea kupambana, lakini kazi ya Bunge Maalumu itaendelea na ndugu zangu Watanzania mjue tunaandaa Katiba safi na rafiki kwa wananchi na itapatikana.”
Sitta alisema baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ya kesi ya Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kumekuwa na tafsiri alizosema ni potofu.
Baada ya maelezo hayo alimpa ruksa AG, Jaji Frederick Werema kutoa ufafanuzi.
Jaji Werema alisema Mahakama Kuu, katika kutafsiri kifungu cha 25(1) (2) inakiri kwamba kuna tofauti kati ya kifungu kilichoandikwa Kiswahili na kile kilichoandikwa Kiingereza.
Alisema Mahakama Kuu katika hukumu hiyo imesema mamlaka ya kuandika Katiba Mpya ina maana ni mamlaka ya kuandika na kupitisha katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Takukuru yalitesa Bunge
Wakati hayo yakiendelea suala la kuingizwa ama kutoingizwa kwenye katiba, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), linaonekana kulitesa Bunge la Katiba baada ya kamati 10 kati ya 12 kulirejesha tena jana.
Rasimu iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ililiacha suala hilo kwa maelezo kuwa siyo moja ya mambo ya Muungano na msimamo huo ukaungwa mkono na Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo.