Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameisifu hatua ya kukamatwa nchini Ubelgiji kwa kamanda mwanamke aliyekuwa katika kikundi cha waasi cha Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor.
Kamanda huyo amekamatwa kwa makosa ya jinai aliyoyafanya wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia.
Hatua ya kukamatwa kwa kamanda huyo, imekuja baada ya malalamiko kuwasilishwa kwa niaba ya waathiriwa watatu wa vita hivyo, mwaka 1992.
Martina Johnson, bado hajatoa jibu lolote kwa madai yaliyowasilishwa mahakamani dhidi yake yakiwemo kuwaua watu kinyama na kuwakatakata vipande
Taylor amefungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita nchini Siera Leone.
Mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa ilimpata na hatia Taylor mwaka 2012 kwa kosa la kusambaza silaha kwa waasi nchini Siera Leone huku naye akipewa madini ya Almasi na waasi hao.
Alianzisha uasi nchini Liberia mwaka 1989 na hatimaye kuwa Rais mwaka 1997 lakini akalazimika kukimbia nchi hiyo baada ya kundi lengine la waasi kuanzisha uasi mwaka 2003.
Shirika moja mjini Geneva, ambalo lilisaidia kufikisha kesi dhidi ya Bi Johnson mahakamani, limesema kwamba tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia mwaka 2003, hakuna juhudi zozote zimefanywa kuchunguza na kufikisha mahakamani kesi za uhalifu uliotendwa wakati wa vita nchini Liberia.
Hii ni licha ya mapendekezo yaliyotolewa mwaka 2009 na tume ya ukweli na maridhiano ya Liberia.