Mwanaume mmoja mkoani Katavi anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kumpiga nyundo kichwani kisha kuufungia mwili wa marehemu ndani ya nyumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea kijijini hapo Septemba 14, mwaka huu saa 1.30 asubuhi ambako mwanamke aitwaye Bernadeta Bwetel (38) mkazi wa Kijiji cha Uruwila Wilaya ya Mlele aliuawa.
Alisema kabla ya kifo hicho, enzi za uhai wake mwanamke huyo alikuwa akiishi pamoja na mume huyo na watoto wao wawili lakini mume wa marehemu alikuwa na mazoea ya kumpiga mara kwa mara.
Kidavashari alisema siku ya tukio, majirani zao Raphael Antony na Albert Mayamba wakielekea shambani walipita jirani na nyumba ya marehemu, walishtushwa na hali ya hapo ilivyokuwa, tofauti na siku zote ambazo huwa wanaikuta familia hiyo ikiwa hapo nyumbani na kuhisi kuna tatizo.
Majirani hao walikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji, ambaye aliongozana nao hadi kwa Mtendaji wa Kata, Didasi Buyaga.
Alisema baada kufika nyumbani kwa marehemu, walikuta mlango umefungwa kwa kamba kama ishara ya kuonyesha ndani ya nyumba hiyo hakuna mtu.
“Walipiga hodi lakini hawakujibiwa ndipo walipoamua kuvunja mlango na kuingia ndani na kukuta mwili wa marehemu ukionekana alipigwa na kitu kizito kichwani kinachodhaniwa kuwa ni nyundo lakini hawakumkuta mumewe wala watoto na hadi sasa hawajulikani waliko,” alisema.