Na. Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma. Watu wawili wameuawa Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema tukio la kwanza limetokea mnamo tarehe 20/09/2014 majira ya saa 23:30hrs katika Kijiji cha Mzogole Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma ambapo mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la MWAJUMA D/O CHOMOLA mwenye umri wa miaka 48, Mgogo mkazi wa Mzogole aliuawa kwa kupigwa na Rungu tumboni upande wa kushoto na mumewake aliyefahamika kwa jina la RICHARD S/O KODI mwenye umri wa miaka 55, Mhehe mkulima na mkazi wa kijiji cha Mzogole Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma ambaye nae aliuawa tarehe 21/09/2014 majira ya saa 09:00hrs baada ya kushambuliwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi na alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa baada ya wananchi hao kupata taarifa kuwa mwanamke huyo kafariki kutokana na kipigo cha mume wake.
Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kwani RICHARD aliuawa na wananchi baada ya kumuua MWAJUMA ambaye alikuwa mkewake aliyekuwa akiishi nae, baada ya kuchelewa kurudi kutoka kwenye sherehe iliyokuwa hapo kijijini akidhani kuwa ameenda kwenye masuala mengine.
Aidha Kamanda MISIME amesema wananchi waliojichukulia sheria mkononi bado wanatafutwa ili wafikishwe mahakamani.