Polisi mkoani Arusha imemuua kinara namba mbili wa ujambazi wa kuua na kupora wanawake, Wecensilaus Matei(32), maarufu Mandela, Jacob au Star.
Jambazi huyo anadaiwa kushirikiana na jambazi aliyeuawa hivi karibuni, Ramadhan Abdallah (37), maarufu ‘Ramandonga’.

Akithibitisha kuuawa kwa jambazi huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema Mandela alikuwa anasakwa kwa muda mrefu na aliuawa jana saa 10 alfajiri akiwa ndani ya nyumba ya bibi kizee eneo la Nduruma, Arumeru.

Alisema aliuawa katika majibizano ya risasi na polisi waliomtaka kujisalimisha na kukataa ndipo walipolazimika kuvunja mlango wa nyumba na alipotoka alianza kuwarushia risasi polisi.

Alisema wakiwa njiani kumpeleka hospitali ya Mkoa ya Mt Meru walimuhoji na kukiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi akiwa dereva wa pikipiki ambapo pia aliwataja watu waliokuwa wakimsaidia kufanya uhalifu huo ikiwemo aliyemnunulia pikipiki, James Lyatuu (36), ambaye ni mfanyabiashara wa vyuma chakavu.

Jambazi huyo amekuwa tishio kubwa jijini Arusha na ameshafanya matukio mengi ya ujambazi ikiwemo la Agosti 6, mwaka huu saa 3.00 usiku eneo la kwa Iddi, alimuua kwa risasi Shamimu Rashid na Agosti 21, 2014 saa1.00 usiku katika eneo la Olasiti, alimuua kwa kumpiga risasi mtoto Christene Nelson.

Wakati huo huo, polisi inamshikilia mkazi mmoja wa Murieti jijini hapa, Amon Losioku (32), kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mdogo wake Francis Losioku kwa kumchoma kisu shingoni.

Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, katika tukio hilo baba mzazi wa marehemu, Losioku Veneti (70), alifariki dunia baada ya shuka alilokuwa amevaa kunasa kwenye mlango.

 
Top