Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
Pia, aagiza wazawa kuboresha huduma za watalii, vinginevyo atawaruhusu wageni.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemuondoa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungulo na kutoa maagizo mazito kwa kampuni za wazawa.
Maghembe amemuondoa Lufungulo Kinapa na kumrudisha makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) baada ya kufanya mabadiliko kwenye baadhi ya hifadhi hizo nchini na nafasi yake kuchukuliwa na Betrita Loibooki aliyekuwa Mkuu wa Hifadhi ya Arusha.
Pia, Maghembe ametoa muda hadi Mei, mwaka huu kwa kampuni za wazawa zinazohudumia watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kuboresha huduma, vinginevyo ataruhusu ushindani wa kibiashara.
Vilevile, amezitaka kampuni za utalii kuwalipa wapanda mlima mishahara waliyokubaliana na Serikali na hataki kusikia wanapunjwa ujira wao.
Waziri huyo alitoa maagizo hayo katika kikao cha wadau wa utalii wanaohudumia watalii Mlima Kilimanjaro na kusisitiza kuwa wasipoboresha huduma kwa kiwango cha kimataifa, ataruhusu ushindani na kampuni za nje.
Mbali na kufanya mabadiliko hayo, ameuagiza uongozi wa Tanapa kufanya haraka mabadiliko ya watumishi waliopo sehemu za kuingilia watalii za Kinapa.
Profesa Maghembe alisema sababu nyingine iliyochangia kushuka kwa idadi ya watalii ni wageni kupata huduma duni ikiwamo chakula ambacho hakina hadhi ya kimataifa.
“Nataka niwaambie, kuanzia mwezi Mei kama hamjaboresha chakula kwa watalii, mishahara kwa wapanda milima na kuwapa mavazi ya kujikinga na baridi nitaruhusu ushindani,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, aliahidi kuitisha kikao cha wadau wote wa utalii kabla ya Mei ili kujadili changamoto na maagizo hayo ya waziri.
Msemaji wa Wapanda Mlima Kilimanjaro na Meru, James Mwamatego alisema kwa muda mrefu wameomba kupatiwa mikataba ya ajira, lakini baadhi ya wamiliki wa kampuni za utalii wamegoma. Mwenyekiti wa Chama cha Huduma za Utalii Mkoa wa Kilimanjaro (Kiato), Amos Lufungilo alisema wapo baadhi ya raia wa kigeni wanaomiliki nyumba ‘bubu’ za kulala wageni na kufanya biashara ya kuongoza watalii.