Rais John Magufuli
Kauli hiyo ya Peneza aliyotoa wakati akichangia mjadala wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, iliamsha hisia tofauti kwa wabunge na kumlazimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kuingilia kati na kutoa ufafanuzi.
Dodoma. Mjadala ulioibuka baada ya Rais John Magufuli kuanika hadharani mshahara wake wa Sh9.5 milioni kwa mwezi, jana ulihamia bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza kuhoji sababu za mshahara huo kutokatwa kodi kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Serikali.
Kauli hiyo ya Peneza aliyotoa wakati akichangia mjadala wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, iliamsha hisia tofauti kwa wabunge na kumlazimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kuingilia kati na kutoa ufafanuzi.
Hivi karibuni, Dk Magufuli alitaja mshahara wake huo huku akiahidi kuwa atatoa nyaraka (salary slip) zinazoonyesha mshahara huo punde akitoka mapumzikoni wilayani Chato mkoani Geita.
Uamuzi huo wa Rais Magufuli ulikuja baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mwenzake wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kumpa changamoto ya kutaja mshahara wake.
Changamoto hiyo ilifuatia kauli ya Rais ya kukusudia kufyeka mishahara ya wakuu wa taasisi za umma kutoka karibu Sh40 milioni kwa mwezi mpaka Sh15 milioni.
Dk Magufuli alifichua siri hiyo ya mshahara kwenye kipindi cha uchambuzi wa magazeti cha 360 kinachorushwa Televisheni ya Clouds, baada ya watangazaji kusoma habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku kuwa Zitto na Lissu wamemtaka ataje mshahara wake ili ukatwe kodi.
Jana, Peneza alitaka mshahara huo ukatwe kodi ili kiongozi huyo mkuu wa nchi awe mfano kwa wananchi: “Kama anataka kuongoza kwa mfano, basi mshahara wake ukatwe kodi ili wananchi waone kuwa wanaongozwa na Rais anayeishi katika mifano na uhalisia.”
Kabla ya kutoa kauli hiyo, mbunge huyo alianza kwa kueleza tofauti na uongozi wa Rais Magufuli na Mwalimu Julius Nyerere, akisisitiza kuwa Nyerere alikuwa alifanya mambo yake kwa uwazi zaidi.
Kauli hiyo ilimnyanyua Simbachawene aliyeomba taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na kufafanua kuwa mshahara wa Rais hauwezi kuhojiwa huku akinukuu Ibara ya 43 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoeleza masharti ya kazi ya Rais.
Ibara hiyo inasema: “Mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.”
Hata baada ya kupewa taarifa hiyo, Peneza aliendelea kusisitiza kuwa lengo lake ni mshahara huo kukatwa kodi kwa maelezo kuwa Rais anapaswa kuwa mtu anayeishi kwa mifano ili atakaporejea kwa wananchi na kuwataka wafanye jambo fulani, iwe rahisi kutekelezwa.
Kauli hiyo ilizua minong’ono bungeni kutokana na wabunge kuonekana wakijadiliana chinichini kabla ya Spika Ndugai kumnyanyua mchangiaji mwingine wa mjadala huo wa mpango wa maendeleo.
Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe pia aligusia suala hilo akisisitiza kuwa mjadala huo umeibuliwa na Dk Magufuli mwenyewe ndiyo maana unajadiliwa.
CREDIT:MWANANCHI