Tarehe 27 na 30 Aprili, 2015, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ilitangaza ajira ya wahitimu wa mafunzo ya ualimu na mafundi sanifu wa maabara kwa kuweka orodha kwenye tovuti ya www.pmoralg.go.tz. Iliagizwa kuwa waajiriwa wapya walipaswa kuripoti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzia tarehe 01 hadi 09 Mei, 2015.
Napenda kuchukua nafasi hii kuutaarifu umma kuwa ofisi yangu ilipokea na kuchambua maombi ya walimu ambao hawakuajiriwa awali; na walioomba kubadilishiwa vituo kutokana na matatizo mbalimbali.

Vilevile ofisi imezingatia kuwapanga tena walimu ambao kwa sababu za msingi walishindwa kuripoti kufikia tarehe 09 Mei, 2015. 

Walimu wote waliopo katika orodha ya awamu ya pili wanapaswa kuripoti kuanzia tarehe 01 hadi 05 Juni, 2015 kwenye ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya kuajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi.

Orodha ya walimu hao watakaoajiriwa katika halmashauri husika imegawanywa katika makundi yafuatayo:-

i. walimu wa cheti (Daraja IIIA) waliokosa ajira kwa awamu ya kwanza;

ii. walimu wa cheti (Daraja IIIA) waliobadilishiwa vituo;
iii. walimu wa masomo ya sanaa kwa ajili ya shule za sekondari ambao hawakupangiwa vituo; 

iv. walimu waliobadilishiwa vituo wa masomo ya sanaa kwa ajili ya shule za sekondari; 

v. walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za sekondari ambao hawakupangiwa vituo; na


vi. walimu waliobadilishiwa vituo wa masomo ya sayansi na hisabati kwa ajili ya
shule za sekondari.

Utaratibu wa Ajira ya Walimu Awamu ya Pili
Kila mwajiriwa mpya anatakiwa kuzingatia yafuatayo:-i. kuwasilisha vyeti halisi vya taaluma ya kuhitimu mafunzo ya ualimu, elimu ya sekondari, cheti cha kuzaliwa pamoja na nakala zake; na

ii. atalipwa posho ya kujikimu kwa muda wa siku saba (7) na nauli ya usafiri wa magari (ground travel), malipo hayo yatatolewa na halmashauri husika.

Angalizo
i. Walimu ambao wamekwisharipoti na mchakato wao wa ajira umeanza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hawatahusika na mabadiliko haya hivyo waendelee kufanya kazi katika halmashauri husika na hawahusiki na upangaji wa awamu hii.

ii. Walimu ambao walichelewa kuripoti tarehe 9 Mei, 2015 na majina yao hayajaonekana katika mabadiliko haya wanatakiwa waende kuajiriwa katika halmashauri walizopangwa awali (kwa kuzingatia orodha iliyotolewa kwenye tovuti tarehe 30/4/2015). Aidha, walimu wa masomo ya sanaa ambao hawakuripoti katika Halmashauri za Wilaya za Meru na Arusha wamebadilishwa vituo.

iii. Walimu waliopangwa ni wale wa masomo ya sanaa/biashara na cheti waliohitimu mafunzo kwa mwaka wa masomo 2013/14 na wahitimu wa miaka ya nyuma wa masomo ya sayansi na hisabati kwa ajili ya kufundisha katika shule za sekondari.

iv. Kituo cha kazi cha mwalimu ni shule na sio Makao Makuu ya Halmashauri, posho italipwa baada ya mwalimu kuripoti na kuandika barua kupitia kwa
Mkuu wa Shule.

v. Mwalimu hatapokelewa na kuaajiriwa kama ikitokea yupo katika orodha na amehitimu shahada au stashahada zisizo za ualimu na wenye shahada za ualimu zisizo na somo au masomo ya kufundishia katika shule za sekondari.

vi. Ikibainika kuna mwalimu atakayekwenda kuripoti na kuchukua posho na kuondoka, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

Ni muhimu kuzingatia maelekezo haya, ikiwa ni pamoja na muda uliowekwa kuripoti kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Limetolewa na
Ndg. Jumanne A. Sagini
KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU-TAMISEMI 
______________













 
Top